Mgombea urais ADC azindua kampeni Mwanza, aahidi mabadiliko

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 07:48 PM Sep 07 2025
 ADC yaahidi mabadiliko
PICHA: VITUS AUDAX
ADC yaahidi mabadiliko

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe, amezindua rasmi kampeni zake Jijini Mwanza huku akitoa ahadi kabambe za kuleta mabadiliko ya kweli nchini endapo atapewa ridhaa na wananchi kuingia Ikulu.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza,  Mulumbe alieleza kuwa moja ya changamoto kubwa nchini ni hali mbaya ya makazi ya askari wa Polisi ,aliahidi kuwa serikali yake itakapochukua madaraka, nyumba zote za askari zilizojengwa tangu miaka ya 70 zitabomolewa na kujengwa nyumba mpya za kisasa, zenye hadhi na staha kwa watumishi hao muhimu wa usalama wa taifa.

“Askari wetu wanastahili kuishi katika mazingira bora makazi yao hayawezi kuendelea kuwa ya dhiki na fedheha,” alisema Mulumbe. Aidha katika sekta ya kijamii, mgombea huyo wa ADC aliahidi elimu na huduma za afya kuwa bure kwa Watanzania wote, sambamba na kuunganishiwa umeme na maji bure kote nchini. Alisema serikali ya ADC itasimama imara kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo za msingi bila mzigo wa gharama kubwa.

“Wajibu wa serikali ni kuhakikisha watu wake wanapata maji safi na salama tutaondoa tozo zisizo na msingi ,Elimu itakuwa bure,  kuunganishiwa maji ni bure ila kutakuwa na mchango mdogo kwa ajili ya kuendeleza mfumo huo,” alifafanua.

Pia akigusia suala la uchumi, Mulumbe aliahidi kufufua viwanda vilivyokufa, kuongeza ajira kwa vijana, na kuhakikisha bidhaa muhimu kama samaki na vifaa vya uvuvi vinashuka bei kwa kupunguza au kuondoa kabisa kodi zinazowakandamiza wavuvi.

“Jana niliagiza samaki hotelini, nikashangaa bei ni shilingi elfu 30! Ziwa lipo hapo mbele yetu! Tukiingia madarakani, tutashusha bei ya samaki na bidhaa nyingine zote za uvuvi kwa kuondoa kodi kandamizi,” alisema

Aidha Mulumbe aliwahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa chama cha ADC katika nafasi zote za uongozi, akisema kuwa wagombea wa chama hicho wapo tayari kutunga sheria rafiki na zisizokandamiza wananchi. Aliongeza kuwa ADC ni chama makini, chenye sera bora na dira ya kweli ya maendeleo.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa ADC, Shoka Juma, aliahidi kuwa serikali ya ADC itatoa mikopo isiyo na riba kwa wananchi wote bila ubaguzi.

“Sasa hivi mikopo inatolewa kwa makundi maalum tu. Wanaume wengi hawafikiki na mikopo hiyo. ADC tutahakikisha kila Mtanzania mwenye sifa anapata mkopo bila riba awe mwanaume, mwanamke au kijana,” alisema.

Hivyo viongozi hao waliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao na kuiamini ADC kama chaguo sahihi la mabadiliko ya kweli, wakisisitiza kuwa wakati wa mabadiliko ni sasa.