RAIS Samia Suluhu Hassan, anaanza ziara ya kiserikali ya siku tatu katika Jamuhuti ya Angola, kwa mwaliko wa Rais João Manuel Gonçalves Lourenço.
Akiwa nchini humo atafanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, atahutubia bunge, kutembelea kiwanda cha mafuta Luanda na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MoU).
Ziara hiyo inaanza Aprili 7 hadi 9, mwaka huu, lengo likiwa na kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya Tanzania na Angola.
Pia atahutubia Bunge la Angola, kuweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu wa Muasisi wa Taifa hilo Hayati Rais António Agostinho Neto pamoja na kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.
"Uhusiano wa Tanzania na Angola uliasisiwa na Waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais António Agostinho Neto, waliokuwa na maono ya pamoja ya kuikomboa Afrika na watu wake," imesema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu.
Aidha, uhusiano huo umeendelea kuimarika siku hadi siku na sasa unajikita katika kukuza uchumi hasa katika sekta za biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, mafuta na gesi, madini, uchumi wa buluu, afya, elimu na utalii kama zilivyoainishwa kwenye Tume ya pamoja ya Ushirikiano."
Rais Samia pia atashuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.
Pia, Rais Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira, ambae nae pia ni mwanamke, kuhutubia Bunge la nchi hiyo na atakuwa ni Rais wa kwanza Mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.
"Ikumbukwe kwamba ziara hii inakuja miaka 19 tangu Maraisi wa Tanzania kufanya ziara za Kiserikali nchini humo ambapo ziara ya kwanza ilifanywa na Baba wa Taifa, ikifuatiwa na Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2006, pia alihutubia Bunge la nchi hiyo kama Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU),"
Aidha, Rais Samia atahitimisha ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.
"Angola ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na uchumi wake unaendeshwa zaidi na mafuta. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya gesi barani Afrika.
“Hii inatoa fursa kwa nchi hizi mbili kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na kujenga uwezo wataalamu wake," imefafanua taarifa hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED