Serikali kujenga minara sita wilayani Mwanga kuimarisha mawasiliano

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 11:28 AM Apr 13 2025
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Jerry Silaa akizungumza na wananchi wilayani Mwanga.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa akizungumza na wananchi wilayani Mwanga.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inajenga minara 38 kwa ruzuku ya Sh. bilioni 7.1 mkoani Kilimanjaro ikiwemo minara 6 inayojengwa katika wilaya ya Mwanga kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika.

Waziri Silaa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha Karamba Ndea,  kata ya Toloha wakati wa ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, hususani katika lango la kuingia na kutoka watalii la Ndea kwenye hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. 

Silaa ameongeza kuwa, minara hiyo sita inayojengwa katika wilaya ya Mwanga, itasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma ya mawasiliano ya simu katika lango hilo na kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla.

wamama.jpeg 496.95 KB

Akizungumzia wananchi kuunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti, Silaa amesema, Serikali imekamilisha mradi wa kuiongezea uwezo (upgrade) minara 468 nchini iliyokuwa imejengwa kwa teknolojia ya kizazi ya pili (2G) ambayo hutoa huduma za kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi, kwenda teknolijia ya kizazi cha tatu na cha nne yaani (3G) na (4G), ambazo zinawezesha wananchi kutumia huduma ya intaneti kupitia simu zao.