ORODHA ya watu matajiri barani Afrika ya Forbes 2024 ilifunua kwamba utajiri wake uliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.5 hadi dola bilioni 1.8, akiwa ni bilionea pekee anayejulikana hadharani katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Alipangwa katika nafasi ya 12 barani Afrika, akifungana na Strive Masiyiwa, mzaliwa wa Zimbabwe na mkazi wa London. Mfanyabiashara Mohammed Dewji, maarufu Mo, ameibadilisha Simba kuwa klabu ya kiwango cha juu barani Afrika.
Mchango wake si katika biashara na uhisani pekee, bali pia kwenye soka la Tanzania kupitia klabu hii ya Simba. Kama Rais na mwekezaji mkuu, MO Dewji amesimamia mageuzi makubwa yaliyoipeleka Simba SC kutoka nje ya nafasi 100 bora hadi nafasi ya saba (7) barani Afrika.
Mabadiliko aliyoyaongoza ni makubwa — kutoka kwenye mchakato wa kuikuza kitaswira (rebrand) klabu hiyo na kutambulisha nembo mpya hadi kuhakikisha wachezaji wanalipwa mishahara rasmi.
Mo alihakikisha kuwa wachezaji hawapati tena mishahara midogo ya Sh. 50,000, bali wanahamasishwa kwa mazingira bora ya kazi yao.
"Mpira si kuhusu kushinda pekee; ni kuhusu kuhamasisha vijana na kutoa fursa zinazoleta mabadiliko ya kweli," anasema Mo, Simba ikiwa ni klabu pekee ya ukanda wa CECAFA iliyosalia katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, ikiwa katika hatua ya robo fainali.
Kupitia taasisi yake ya Mo Dewji Foundation, mfanyabiashara huyo pia ameahidi kutoa nusu ya utajiri wake kwa misaada, akifuata mafundisho ya imani yake. Anajivuania mabadiliko makubwa kwenye afya, elimu na upatikanaji huduma ya maji safi kwa jamii za pembezoni.
"Nilifundishwa na wazazi wangu kuwa uhisani ni wajibu, si chaguo," anasema Mo ambaye amekuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa barani Afrika kwa muda mrefu.
KUTENGENEZA AJIRA
Katika hatua mpya ya safari yake — ikiwa na ongezeko kubwa la thamani kati ya dola milioni 400–500 kwa mujibu wa Forbes, Mo anatazama mbali
zaidi ya ukubwa wa utajiri wake, akilenga kuonesha athari pana za mchango wake katika jamii.
Akiwa mtu wa imani, mfadhili wa kujitolea, na mwekezaji mwenye maono, anasema ana shauku kubwa ya kujenga nafasi za ajira, kupanua biashara zake kimkakati na kurudisha kwa jamii kupitia taasisi yake.
Anasema kampuni zake zinaendelea kupanua biashara zake kimataifa, zikiwekeza katika sekta mpya kama teknolojia na mali isiyohamishika, huku zikiimarisha misingi yake katika kilimo, viwanda na usambazaji. Wakati huohuo, shughuli za uhisani wa Mo zinapanuka zaidi, kupitia ushirikiano wa kimataifa na taasisi kama Chuo Kikuu cha Georgetown, taasisi yake inaendelea kuleta athari chanya katika nyanja za afya, elimu na upatikanaji maji safi kwa wale wanaohitaji zaidi.
“Nina mapenzi makubwa na Tanzania," anasema Mo, "lakini ni wakati sasa wa dunia kutambua kuwa Afrika inaweza kutoa kampuni kubwa za kimataifa — kampuni na viongozi wenye athari ya kweli duniani kote. Kwa mtazamo sahihi, tunaweza kupeleka maadili yetu ya mshikamano, huruma na ukarimu katika jukwaa la kimataifa."
Mfanyabiashara huyo amewekeza katika nchi 11 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Mo anajulikana kwa kuwekeza katika sekta ngumu — kama viwanda vya nguo na kilimo, ambavyo mara nyingi huepukwa kwa sababu ya hatari zake. Kwa kutambua fursa zilizokuwa hazijatumika, aliokoa mashamba ya mkonge yaliyokuwa yameachwa, akieleza kuwa “uzalishaji nyuzi za mkonge kwa kiwango kikubwa ni kama kuchapisha pesa”.
“Ninataka nikumbukwe si kwa kiasi cha pesa nilichopata, bali kwa maisha niliyobadilisha,” anasema Mo anayeamini biashara inaweza kuwa chombo cha mabadiliko chanya kutoka kujenga viwanda na kuzalisha ajira hadi kusaidia jamii kupitia uhisani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED