BARAZA la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) limemtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (AG) kuondoa kesi zote dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, na kumuachia huru kuendelea na majukumu ya kujenga demokrasia na maendeleo kwa ustawi wa nchi yetu kwa kuwa kudai mabadiliko ya sheria za kiuchaguzi si uhaini wala uasi.
Taarifa kwa umma iliyotolewa Aprili 13,2025 na Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa, Sharifa Suleiman, wamelaani kukamatwa kikatili na kusomewa mashtaka ya uhaini na uchochezi akiwa wilayani Mbinga Aprili 10,2025.
"Mwenyekiti kukamatwa na kupewa kesi hizo hazitaififisha BAWACHA kusukuma agenda kuu za chama za sasa za 'No Reforms No Election', 'Stronger Together' na 'Tone Tone'.
Aidha, amesema BAWACHA wanaunga mkono chama kutokwenda kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, Ubunge na Udiwani, ikiwa ni mwendelezo wa kusimamia ajenda ya chama ya sasa.
Kwa mujibu wa BAWACHA, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni miongoni mwa maeneo yenye dosari kubwa na inahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka.
"Baraza linatoa wito kwa BAWACHA nchi nzima kuungana na chama katika operesheni 'No Reforms No Election', sambamba na ajenda za 'Stronger Together' na 'Tone Tone'.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED