KASI ya mfumuko wa bei kwa mwaka kutoka Aprili 2023 hadi Aprili 2024, imepungua kufikia asilimia 4.88 kutoka asilimia 4.92 iliyorekodiwa Machi, mwaka huu pekee.
Mkuu wa Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Hassan Jamal Hassan, alisema jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari, Mazizini, nje ya mji wa Zanzibar.
Alisema bidhaa zilizosababisha kupungua kwa mfumko wa bei na asilimia kwenye mabano ni mchele wa Mbeya (11.5), unga wa ngano (3.0), unga wa sembe (7.5), mafuta ya kupikia OKI (5.6), ndizi za mkono mmoja (21.3) na ndizi za mtwike (30.4).
Alisema kwa ujumla faharisi za bei zimeongezeka na kufikia 111.42 kwa mwezi Aprili 2024 ikilinganishwa na 106.24 ambayo iliripotiwa katika mwezi kama huo mwaka jana.
Hassan alisema kundi la bidhaa za chakula na vinywaji visivyo na kileo kwa Aprili, 2024 zimeongezeka na kufikia asilimia 7.82 ikilinganishwa na asilimia 7.38 iliyorikodiwa katika mwezi wa Machi 2024.
Kwa upande wa mfumuko wa bei Aprili, mwaka huu, umeongezeka na kufikia asilimia 1.81 ikilinganishwa na asilimia hasi 0.09 iliyorikodiwa katika kipinjdi kama hicho, mwaka jana.
Pia alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za chakula na vinywaji visivyo na kileo kwa Aprili, 2024 umeongezeka na kufikia asilimia 3.80 ikilinganishwa na asilimia hasi 0.51 iliyorikodiwa katika Machi, mwaka huu.
Meneja Msaidizi – Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Zanzibar, Shamy Chamicha, alisema kupungua kwa kasi ya mfumuko wa bei ni hatua nzuri ya kiuchumi na malengo yaliokuwepo ya kubakia kwenye tarakimu moja.
"Ni ahueni kwa wananchi na hii inatokana na kuwepo kwa bidhaa za kutosha kwenye masoko. Lakini kwa ujumla hali ya uchumi imeendelea kubakia vizuri na hata upatikanaji wa dola hivi sasa upo vizuri," alisema.
Mfumuko wa bei wa Zanzibar ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazokusanywa katika masoko ya miji ya Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED