Katika kongamano la nne la Operesheni Linda Demokrasia lililofanyika mkoani Songwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, ametuma ujumbe mzito kwa serikali ya CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kiko tayari kuongoza harakati za kweli za kidemokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Akihutubia wanachama na wapenzi wa chama kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine, Dorothy Semu aliwapongeza kwa moyo wao wa kujitolea na kusimama kidete katika kulinda demokrasia. Alisema kuwa kongamano hilo si mkutano wa kawaida, bali ni wito wa kihistoria kwa Watanzania wote kuamka na kusimama kwa ajili ya haki, usawa, na uhuru wa kweli.
Mapambano ya Demokrasia Yanaendelea
Dorothy Semu alieleza kuwa kongamano hilo linajengwa juu ya msingi thabiti wa mikutano mingine mitatu iliyofanyika Dar es Salaam, Lindi, na Kigoma, inayoonesha nia ya dhati ya chama hicho kujenga mfumo wa haki katika siasa za Tanzania. Alifafanua kuwa Operesheni Linda Demokrasia ni zaidi ya kampeni ya kisiasa ni harakati ya ukombozi wa kisiasa nchini.
Akitaja changamoto zilizokumba uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, Semu alilaani vitendo vya uvunjifu wa haki na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wapinzani. Alitoa mfano wa kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Songwe, Ndugu Zambi, pamoja na kushambuliwa kwa Katibu wa Mkoa, Ndugu Kelvin, huku akisema matukio hayo yanaonesha wazi jinsi chama tawala kilivyopoteza dira ya haki.
“Je, CCM inaweza kweli kujivunia ushindi unaotokana na mateso ya wananchi?” alihoji Semu. “Hii sio demokrasia – ni udikteta uliovaa suti ya uchaguzi.”
Hakuna Kurudi Nyuma – ACT Wazalendo Imara
Katika hotuba yake yenye msisimko mkubwa, Dorothy Semu alisisitiza kuwa chama chake hakitakubali hofu kuwa silaha ya kuwavunja moyo Watanzania. Alieleza kuwa ACT Wazalendo iko tayari kuongoza "uasi wa haki" dhidi ya mifumo ya ukandamizaji, huku akimpongeza Tundu Lissu wa CHADEMA kwa kusimama kidete licha ya changamoto za kisiasa.
“Mashtaka dhidi ya Lissu hayatuzuii – yanatupa nguvu zaidi ya kuendelea! Niko tayari kuongoza mapambano haya kwa niaba ya Watanzania wote,” alisema kwa msisitizo.
Madai Sita ya Msingi kwa Uchaguzi Huru na Haki
Dorothy Semu aliweka wazi madai sita ya msingi ambayo ACT Wazalendo inapigania kupitia Operesheni Linda Demokrasia. Madai hayo ni Makamishna wa Tume ya Uchaguzi wajiuzulu na wateuliwe upya kwa mujibu wa sheria, Mawakala wa vyama wawe huru na wapate fomu za matokeo bila kizuizi. Wagombea wasienguliwe bila sababu za msingi, Kudhibiti kura feki. Wakurugenzi wa Halmashauri wasihusike kama wasimamizi wa uchaguzi na pia vyombo vya ulinzi visitumike kuvuruga uchaguzi.Akitilia mkazo madai hayo, Semu alisema sio magumu.
“Madai haya sio magumu – yanahitaji tu uamuzi wa kisiasa. CCM wanajua kuwa wakishindana kwa usawa, hawana nafasi ya kushinda.” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED