KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema wanatambua katika vyama vya ushirika wako mchwa na wabadhirifu ambao ndio wakushughulikiwa.
Makalla ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Amesema amefurahi kupokea taarifa kutoka kwa Ofisa Ushirika Mkoa, ambapo jitihada za serikali ni kusaidia vyama vya ushirika na wakulima katika kupata bei katika kuongeza pembejeo na kusababisha maisha ya watu kubadilika siku hadi siku.
“Nyie ni mashahidi wakati wa kangomba bei ya korosho ilikuwa shilingi ngapi na sasa ni shilingi ngapi, hatua ni kubwa. Wenzetu waliambiwa huko Nachingwea na hao waliosema huku mbali, kwamba ushirika huu hauna maana, jana nilieleza Kilwa katika wale viongozi wanaopotosha wananchi hakuna hata mwenye shamba, hawajui kulima na hawajui mazao haya,” anasema.
Aliwaomba wananchi waendelee kushirikiana na serikali, kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan, ameingia katika rekodi ya kubadilisha maisha ya wakulima, kuongeza ruzuku ya pembejeo ya mbegu na mbolea.
“CCM kwenye ilani tumeongeza mipango yetu kuboresha ushirika, hao wengine hawana dhamana wala wajibu, wasikilizeni viongozi wenu.
“Tunatambua wapo mchwa na watu wabadhirifu kwenye vyama vya ushirika, hao ndio watu wa kushughulika nao kwenye ushirika ili uendelee kuwa na nguvu na kuendelea kuwasaidia wakulima.
“Kama ni pembejeo zinatoka ziwafikie wakulima wasijinufaishe watu wachache, hao ndio wakula nao sahani moja.
“Kwa hiyo tuko macho, Mkuu wa Mkoa yuko macho, Mkuu wa Wilaya yuko macho, CCM iko macho, lengo letu ni kuhakikisha wananchi wetu, wakulima wetu kupitia ushirika wanaimarika zaidi na mazao yao yanakuwa na tija na kuwasaidia katika kuboresha uchumi na maisha yao,” amesema.
Amesisitiza kuwa hayo ndiyo mambo yaliyowafanya wananchi wakiamini Chama Cha Mapinduzi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED