Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhan, ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mwaka 2025, chama ambacho hakitasaini maadili hayo hakitashiriki uchaguzi mwaka huu na chaguzi zingine zote ndogo zitakazofanyika kwa muda wa miaka mitano.
Vyama vya siasa 18 kati ya 19 ndivyo vimesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi 2025 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakijasaini.
Akizungumza katika hafla ya kusaini kanuni za maadili, Kailima ameeleza wajibu wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi kwa mujibu wa kifungu namba 162(2) cha sheria hiyo pamoja na aya ya 1.2 ya kanuni za maadii ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, kanuni zinapaswa kusainiwa na wahusika kwa kila chama cha siasa, serikali na Tume.
“Maadili ya uchaguzi ni muhimu katika kuwezesha uchaguzi huru na haki ni muhimu kwa pande zote kuhusika na kusaini maadili hayo, mchakato wa maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani hushirikisha wadau na tunawashukuru wadau wote kwa maoni mliyotoa wakati wa maandalizi ya kanuni hizi," alisema.
Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mrema alipoulizwa kuhusu ushiriki wao katika mchakato wa uchagzui ikiwa chama chao hakijatia saini kanuni hizo za maadili alisema watakuna ili kutoa tamko lao na namna watakavyofanya.
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga alipoulizwa alisema bado ni mapema kwake kutoa maoni kuhusu kusainiwa kwa kanuni hizo huku akitabiri chama chake kuporomoka kisiasa.
"Bado ni mapema sana kutoa maoni kwakua ndio imetokea leo. Ila ninakiona chama changu kikiingia kwenye poromoko kubwa sana la kisiasa na kama hatua za haraka hazitachukuliwa basi naona chama changu kikielekea kwenye kaburi ambapo hakitaweza kunyanyuka tena." alisema Mchome
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED