Rais wa Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga, pamoja na dereva wake, Muhajiri Mohammed Haule, waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Bunda, mkoani Mara.
Kupitia salamu zake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo hivyo na kueleza kuwa ni pigo kubwa kwa taifa, hasa katika sekta ya nishati ambayo marehemu Mhandisi Nyamohanga alikuwa akiitumikia kwa bidii na weledi mkubwa.
“Natoa pole kwa familia za marehemu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, watumishi wa TANESCO, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mzito,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amewaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ibada katika kipindi hiki kigumu, akimuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED