Uongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) unatarajia kufanya ziara katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa na lengo la kutangaza mafanikio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan katika sekta ya elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 14, 2025, Katibu Mtendaji wa TAHLISO, Godfrey Gilagu, amesema ziara hiyo itaongozwa na Rais wa Jumuiya hiyo, Geoffrey Kiliba, na itatoa taarifa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Rais, ikiwemo Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation).
“Mradi wa HEET unaogharimu zaidi ya Dola milioni 421 umeendeleza miundombinu katika vyuo takribani 19 nchini. Ni mradi mkubwa na muhimu sana kwetu wanafunzi,” amesema Gilagu.
Ameeleza kuwa ziara hiyo pia inalenga kuwahamasisha wanafunzi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za wanafunzi kwa kupata viongozi makini watakaowatetea na kuchangia maendeleo ya nchi.
Gilagu ameongeza kuwa TAHLISO imejipanga kukabiliana na watu wote wanaopanga kuvuruga uchaguzi huo katika vyuo vikuu, huku akiwahimiza wanafunzi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa wanafunzi mwaka huu.
Aidha, ziara hiyo itahusisha kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi, kuziwasilisha kwenye mamlaka husika, pamoja na kutoa elimu juu ya kulinda amani katika mazingira ya vyuo vikuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED