SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeanza kuhakikisha Watanzania wanapata vyakula ambavyo vina ubora na lishe pamoja na kuwapo kwa virutubishi muhimu kwa ustawi wa afya zao, ili kupambana na tatizo la udumavu na utapiamlo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka TAMISEMI, Luitfrid Nnally, amesema hayo wakati akiwasilisha salamu kwenye mafunzo ya wadau wa wataalamu wa urutubishaji vyakula kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo ya siku nne, yameandaliwa kwa pamoja na Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula Tanzania (The Tanzania Food Fortification Alliance-TFFA), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afya, Taasisi ya Food Fortification Initiative (FFI), Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania chini ya uwezeshwaji wa Shirika la UNICEF.
Nnally amesema kipaumbele hicho kilishawekewa mkakati na Rais Samia Suluhu Hassan, tangu alipokuwa Makamu wa Rais, aliweza kusainisha mikataba na wakuu wa mikoa kuhakikisha jamii inakuwa na lishe bora, ili kupambana na tatizo hilo la udumavu na utapiamlo.
“Tupo hapa kwenye mafunzo, kwa ajili ya kujadili mikakati hii, tumshukuru Rais Samia, ambaye suala la lishe amelipa kipaumbele kikubwa na kauli mbiu yake, ‘Tanzania bila utapiamlo inawezekana’,” amesema Mkurugenzi huyo msaidizi .
Hata hivyo alitumia nafasi hiyo kupongeza jitihada za zilizofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara, kutunga sheria na kupitisha kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula, ili viwe na ubora katika kusaidia kupambana na matatizo ya lishe kwa watoto na jamii ya watanzania .
“Hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais za kuhakikisha kwamba vyakula vina kuwa na ubora wa kusaidia kupambana na matatizo ya lishe kwa watoto na kwa jamii mzima ya watanzania na wakiwa na afya bora wanaweza kuchangia uchumi wa taifa letu,“ amesema Nnally.
Amesema baada ya mafunzo hayo, jukumu kubwa kwa watendaji na wadau mbalimbali wenye mamlaka ni ufuatiliaji kwa wataalamu waongezaji virutubishi kwenye vyakula, ili kuona ubora wa vyakula unakuwa wa viwango vya juu .
Ametaja eneo lingine ni kuangalia wasindikaji wa vyakula endapo wanazingatia viwango vilivyowekwa kitaifa kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa na matokeo mazuri ya kiafya, yanayotokana na ulaji wa vyakula hivyo .
“Tutahakikisha tunafanya ufuatiliaji kwenye maeneo ya ndani ya viwanda au ndani mzalishaji wa hicho chakula kwa kuangaliwa ubora wa malighafi zinazotumika kuongezea virutubishi, mchakato wa usindikaji uzingatie viwango, eneo la uonjaji na kupima ubora wa kile kinachozalishwa,” amesema Nnally.
Eneo lingine ni ufuatiliaji wa nje ambao utafanywa na serikali au mamlaka zinazohusika na uthibiti wa ubora wa chakula kwa kutembeelea maeneo ya uzalishaji kuona uzingatiaji wa vyakula kwenye masoko, mipakani na bandarini kuwa vyakula vyote vinakuwa na ubora uliokubalika.
Nnally alizishauri Taasisi ya Chakula na Lishe pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kupitia maabara zao kuhakikisha wanapima ubora wa vyakula hivyo, ili kuangalia iwapo vina virutubishi wenye usalama kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopitishwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Ofisa Biashara Mwandamizi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Festo Kapela, amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuimalisha afua ya uongezaji virutunishi kwenye vyakula.
Amesema kama nchi tayari, Aprili 3, mwaka huu, zimezunduliwa kanuni ambazo zinaenda kutumika na lengo kubwa ni kuhakikisha unawekwa ulazima katika suala la uongezaji virutubishi kwenye chakula.
Amesema kabla sheria na kanuni hizo, wazalishaji wa vyakula kulikuwa na kulaumiana ya kwamba baadhi walikuwa wakiweka virutubishi, lakini wengine hawaweki na kulifanya jambo kuwa ngumu katika utekelezaji wake.
“Baada ya kanuni kuzunduliwa sasa ni lazima kuongeza virutubishi kwenye chakula na wataalamu wetu kutoka TBS kwa kushirikana na wa TAMISEMI wataanza kupita huko,” amesema Kapela.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo, baada ya kumaliza wakawe mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa wenzao ambao hawakuipata, ili waone ni namna umuhimu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula.
Amesema suala la lishe na chakula linaenda katika nyanja kadhaa kwani ni afya, maisha lakini pia ni uchumi na hivyo kuziomba sekta binafsi zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula kutekeleza suala hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED