Serikali kununua meli za uvuvi wa Bahari Kuu, yapeleka boti za kisasa Ziwa Nyasa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:33 PM Apr 16 2025
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti
Picha: Nipashe Digital
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, amesema serikali ina mpango wa kununua meli maalum kwa ajili ya shughuli za uvuvi katika Bahari Kuu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa bluu na kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi nchini.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Mnyeti amesema sambamba na mpango huo, serikali pia imeweka mkazo mkubwa katika ununuzi wa boti za kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi katika maziwa yote nchini. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kupeleka boti nne za kisasa pamoja na zana za uvuvi katika Ziwa Nyasa.

Akiitikia swali la Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga (CCM), aliyetaka kufahamu iwapo serikali ina mpango wa kupeleka meli ya uvuvi Ziwa Nyasa ili kuvua samaki wanaoishi kwenye kina kirefu, Mhe. Mnyeti alisema tayari hatua zimechukuliwa kupitia upatikanaji wa boti za kisasa zenye uwezo wa kuvua katika maeneo hayo.

"Boti zilizopelekwa Ziwa Nyasa zina urefu wa mita 7.06, mita 10 na mita 12. Kati ya hizo, boti mbili zenye urefu wa mita 10 na moja ya mita 12 zina uwezo wa kufanikisha uvuvi kwenye kina kirefu cha Ziwa Nyasa," alieleza Mnyeti.

Aliongeza kuwa boti hizo zilitolewa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ambapo zilitolewa kwa vikundi vya wavuvi, makampuni binafsi, vyama vya wavuvi, vyama vya ushirika pamoja na watu mmoja mmoja kupitia mikopo isiyo na riba.

Mnyeti alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya uvuvi kwa kutoa vifaa vya kisasa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija kwa wavuvi wa maeneo ya pembezoni, hususan kwenye maziwa makuu kama vile Ziwa Nyasa.