Katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini, visima vipya vitatu vinatarajiwa kuchimbwa katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara ambavyo vitaongeza uzalishaji wa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.
Akizungumza katika ziara ya waandishi wa habari mkoani Mtwara iliyoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), mwishoni mwa wiki, Msimamizi wa uzalishaji wa kampuni ya Maurel et Prom Exploration inayoendesha shughuli za Mnazi Bay, Hussein Chitemo, alisema visima hivyo vinatarajiwa kuanza kuchimbwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
“Visima hivi vipya vinatarajiwa kuzalisha zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku, na gesi hiyo itaongezwa kwenye kiasi cha sasa cha futi milioni 100 zinazozalishwa kutoka visima vitano tulivyo navyo. Majadiliano na maandalizi yako katika hatua za mwisho na tunatarajia kuanza kuchimba kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema.
Chitemo alisema gesi inayozalishwa kutoka visima hivyo husafirishwa kwenda kwenye mitambo ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mtwara na Kituo cha Madimba kinachomilikiwa na GASCO, kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Alisema kuongezeka kwa visima hivyo, kutaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya uzalishaji wa nishati na kukuza zaidi sekta ya viwanda hasa kwa uhakika wa upatikanaji wa gesi asilia.
Mtaalamu wa jiolojia kutoka PURA, Desmond Risso, alisema dhamira ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha sekta ya gesi asilia inaleta manufaa chanya kwenye sekta nyingine za uchumi nchini.
“Tunaongeza juhudi zetu kwa kuwekeza kwenye ushirikiano wa kimkakati na teknolojia za kisasa, sambamba na kuongeza uelewa kwa umma na ndiyo maana tumeandaa ziara hii kwa sababu zinasaidia kuongeza uelewa kwa jamii na tunaamini vyombo vya habari ni nyenzo muhimu inayosaidia kuelimisha umma,”alisema Risso.
Ziara hiyo ilihusisha kutembelea miundombinu muhimu kama mashamba ya gesi ya Mnazi Bay, Kituo cha Muunganiko wa Bomba la Gesi Somanga na Kiwanda cha Kusafisha Gesi cha Madimba kinachoendeshwa na GASCO, Chuo cha Ualimu Mtwara (K) ambako wadau walishuhudia mabadiliko chanya yanayoletwa na matumizi ya gesi asilia kwa kupikia.
Risso alisema kupitia programu ya uelimishaji kwa umma, PURA pia imekuwa ikiunganisha wadau mbalimbali na sekta hiyo lengo likiwa ni kuongeza ushiriki wa wananchi katika kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Joan Ngwale, Ofisa wa Usalama, Mazingira na Uhusiano wa Jamii kutoka Maurel & Prom, alisema ziko fursa mbalimbali ambazo wananchi wanaozunguka eneo la uzalishaji wanazipata katika sekta za elimu, afya na kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na wananchi hao.
“Tunajenga vyumba vya madarasa, tunafadhili wanafunzi, tunajenga vyumba vya kinamama kujifungulia, tunawawezesha wajasiriamali wanaofanya shughuli za kilimo, uvuvi kwa kuwapatia vifaa na na mpaka sasa wapo baadhi ya wanafunzi wanafanya mafunzo kwa vitendo hapa kwetu na wote wanatoka katika maeneo haya,” alisema Ngwale.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED