Mkurugenzi Ilemela akabadhi madawati 25 Mnarani

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:31 PM Apr 16 2025
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu
Picha: Neema Emmanuel
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu ametoa madawati 25 kwa shule ya msingi Mnarani iliyoripotiwa kuwa na upungufu wa madawati ili kuhakikisha wanafunzi hao wanasoma katika mazingira ya kisasa na yaliyobora.

Akimkabidhi madawati hayo kwa Mkuu wa shule hiyo Wayayu leo amesema lengo la serikali ni kuona wanafunzi wanasoma katika mazingira yaliyo bora na yenye kuleta tija.

Wanafunzi wapata madawati 25 Mnarani
Amesema madawati hayo yana uwezo wa kukaliwa na wanafunzi 75 kwa kila dawati moja linakaliwa na wanafunzi watatu lengo likiwa ni kumaliza kabisa adha hiyo.

Mkuu wa shule hiyo Dismas Hamaro amemshukuru  Mkurugenzi  huyo kwa kuipatia shule madawati hayo ambayo yatasaidia wanafunzi kukaa vizuri na kuweza kujifunza vizuri.

Aidha ameahidi ya kutunza miundo mbinu hiyo ya madawati vizuri  ili inufaishe vizazi vingi vitakavyopita  shuleni hapo na viweze kujifunza kwa ufanisi.


"Shule yetu ina wanafunzi 818 ambako kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi walioandikishwa darasa la awali na darasa  la kwanza 2025 kutokana na sera ya Elimu bila malipo na hivyo jamii imekuwa na mwamko mkubwa wa kuandikisha watoto,” amesema Hamaro.

Aidha ametaja kuwa ongezeko hilo limesababisha shule kuwa na upungufu wa madawati na kuwa wamepokea madawati kutoka kwa  Mkurugenzi na wadau mbalimbali akiwemo Desk and Chair Foundation Tanzania hivyo kubaki na upungufu wa madawati 26 pekee.