Vijana na wanawake waoneshwa fursa ufugaji nguruwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:48 PM Apr 16 2025
news
Picha: Mtandao
Nguruwe.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Ufugaji Nguruwe (APICON) litalofanyika Septemba 11-13, 2025 jijini Dar es salaam huku serikali ikijipanga kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake ili kuchoche mageuzi kwenye sekta hiyo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Chama cha Wafugaji Nguruwe Tanzania (TAPIFA) kuandaa kongamano hilo, Naibu Waziri, Alexander Mnyeti, amesema mchango wa nguruwe katika pato la taifa bado ni mdogo na kwamba kupitia kongamano hilo kupanua soko ndani na nje na ushiriki wa watanzania hasa vijana na wanawake kwenye ufugaji huo.

“Jukwaa hili litakutanisha wadau 2,000 kutoka ndani na nje ya Afrika kwa lengo la kuchochea mageuzi katika sekta ya ufugaji wa nguruwe barani Afrika, Pia litaangazia fursa mbalimbali kama ufugaji wa kisasa, matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa masoko ya ndani na ya kimataifa,”amesema.

 

1

Naye, Mwenyekiti wa TAPIFA, Doreen Maro amesema kongamano hilo litafungua milango ya uwekezaji na kuwaasa vijana na wanawake kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ina matokeo ya haraka kiuchumi ikilinganishwa na ufugaji ng’ombe.