Bagamoyo yapanda miti 500 kukabiliana na ukame,kulinda mazingira

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 09:19 AM Apr 16 2025
Bagamoyo yapanda miti 500 kukabiliana na ukame,kulinda mazingira
Picha:Mpigapicha Wetu
Bagamoyo yapanda miti 500 kukabiliana na ukame,kulinda mazingira

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, imefanikiwa kupanda miti zaidi ya 500 katika eneo la mnada wa mbuzi na ng'ombe uliopo Kata ya Zinga kwa Mtoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na changamoto ya ukataji miti ovyo unaosababisha ukame.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti ngazi ya wilaya yaliyofanyika katika eneo hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Stellah Msofe, alisema upandaji wa miti hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, la kutunza na kuhifadhi mazingira.

"Kupitia maadhimisho haya, tumefanikisha upandaji wa miti zaidi ya 500. Lengo letu ni kuurejesha uoto wa asili uliopotea sambamba na kukabiliana na wimbi la ukataji miti ovyo, ambalo limekuwa chanzo kikuu cha hali ya ukame katika maeneo mbalimbali," alisema Msofe.

Msofe aliwahimiza wakuu wa idara, watendaji wa serikali na taasisi binafsi kuendelea kuhamasisha upandaji miti, ili kufanikisha lengo la kitaifa la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Dk. Obed Mwinuka, alieleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kuboresha mazingira, na kwamba eneo hilo la mnada litaendelea kuwa sehemu ya mfano katika utunzaji wa mazingira.

"Kupitia kampeni hii tumepanda miti ipatayo 500 katika eneo hili la mnada wa mbuzi na ng’ombe. Tunaamini hatua hii itaongeza uzuri wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi," alisema Dk. Mwinuka.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo alisema kuwa hadi sasa halmashauri hiyo imefanikiwa kupanda miti zaidi ya 700,000, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kutimiza lengo la serikali la miti milioni 1.5 kwa mwaka.

Mmoja wa wawekezaji katika eneo la mnada huo, Hassan Kashingo, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, ameahidi kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuendeleza jitihada hizo, ikiwa ni pamoja na kuitunza miti yote iliyopandwa.

"Tumejipanga kuhakikisha miti hii inatunzwa vizuri, na tutaendelea kuwa sehemu ya suluhisho katika kulinda mazingira yetu," alisema Kashingo.
3