Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetangaza kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya EXPO 2025 Osaka, yatakayofanyika kuanzia Aprili 12 hadi Oktoba 13, 2025 nchini Japan, ambapo zaidi ya watu milioni 28.2 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kuyatembelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jafo, alisema kauli mbiu ya maonyesho hayo ni “Kuwezesha Jamii kwa Maisha Endelevu” ambayo inalenga kuhamasisha maendeleo shirikishi kwa kutumia ubunifu na teknolojia katika kukuza uchumi wa mataifa.
“Maonyesho haya ni jukwaa muhimu kwa Tanzania kujitangaza kimataifa katika sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, biashara, uwekezaji, utalii, na teknolojia. Kupitia EXPO 2025, nchi yetu inatarajia kupata matokeo makubwa katika uimarishaji wa intelijensia ya taarifa za biashara zitakazoiwezesha Tanzania kutambua fursa za masoko duniani,” ameeleza Jafo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, amesema ushiriki wa sekta binafsi katika EXPO hiyo utajikita zaidi katika kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kuvutia uwekezaji, kukuza utalii, kutafuta wabia wa biashara, na kujifunza mbinu mpya za uendeshaji wa biashara za kisasa.
“Teknolojia na ubunifu vitakuwa nguzo muhimu katika ushiri wa Tanzania, ambapo tutatangaza fursa zilizopo kwenye sekta kama vile Afya, Nishati, Madini, Utalii, Kilimo, Uchumi wa Buluu, Sanaa na Utamaduni,” amebainisha Ngalula.
Aidha, Ngalula alitangaza kuwa kwa kushirikiana na TanTrade, Tanzania imeandaa Kongamano Kubwa la Biashara, Uwekezaji na Utalii litakalofanyika Mei 26, 2025, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya EXPO 2025. Kongamano hilo litatoa fursa kwa wadau wa sekta mbalimbali kukutana na makampuni makubwa yenye nia ya kuwekeza au kushirikiana kibiashara na Tanzania.
“Kongamano hili litahusisha usaini wa hati za ushirikiano kati ya taasisi kutoka Tanzania na Japan, kubadilishana uzoefu, pamoja na kuvutia mitaji ya kibiashara na watalii kuja nchini,” ameongeza.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshiriki kikamilifu katika EXPO 2025 Osaka, ambapo inatarajia kutumia jukwaa hilo kuinua hadhi ya taifa kiuchumi na kidiplomasia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED