ACT Wazalendo: Tutautumia Uchaguzi kama jukwaa la kuitetea demokrasia

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:54 PM Apr 16 2025
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu
PICHA: RAHMA SULEIMAN
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu

CHAMA cha ACT Wazalendo kimetoa sababu tatu kuu zilizowasukuma kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ikiwemo kutetea na kulinda thamani ya kura.

Kimesema uzoefu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unaonesha kuwa thamani ya kura imepotea. 

Akizungumza na waandishi  wa habari visiwani Zanzibar hivi karibuni katika Ofisi za chama hicho Vuga Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu alisema viongozi hawachaguliwi tena kwa kura za wananchi na badala yake ni nguvu ya dola inayoamua nani awe kiongozi wa wananchi. 

"Haya ni mapinduzi dhidi ya haki ya raia ya kuchagua viongozi wao, haki ambayo ndio inadhihirisha uraia wao. Hii ni hujuma isiyovumilika"alisema.

Kiongozi huyo alisema ACT Wazalendo kinafahamu kuwa uchaguzi sio mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi wenyewe, hivyo Chama hicho kwa kutambua dhima kubwa iliyoibeba, kinakusudia kuhamasisha vuguvugu kubwa la wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu 2025 kutetea na kulinda haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Aliongeza kwa kusema" ACT Wazalendo tutautumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama jukwaa la kuitetea na kuilinda demokrasia yetu. Ni vizuri niseme hapa kuwa tumejiandaa kwa hili. CCM ijue kuwa tutaikabili vile itakavyokuja. Tupo tayari kuwaongoza Watanzania kupitia vuguvugu la wananchi kutetea thamani ya kura ili kulinda msingi wa katiba yetu kuwa madaraka yote yanatoka kwa wananchi. Tupo tayari kwa mapambano!

Aidha alisema kususia Uchaguzi kunaimarisha hujuma dhidi ya Demokrasia baada ya tafakuri ya kina, Chama kimejiridhisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinahitaji na kwa hakika kitafurahia iwapo vyama makini vya upinzani vitasusia uchaguzi ili kiendeleze hujuma kwa demokrasia nchini.

Alisema ACT Wazalendo imegoma kutoa fursa hiyo kwa CCM kwa sababu uchambuzi wao unaonesha kuwa katika nchi mbalimbali duniani, kususia uchaguzi kumeimarisha hujuma zaidi za dola dhidi ya demokrasia kwa kutoa mwanya wa kupora kwa urahisi sauti ya wananchi.

"Mifano ya hili inaweza kupatikana kwenye nchi za Kenya (2017), Misri (2018), Ivory Coast (2020), Zanzibar (2015), Venezuela (2018)"alisema.

Alisema ACT Wazalendo inaenda kuutumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama uwanja wa mapambano ya kuzuia hujuma dhidi ya demokrasia na wanakwenda kuutumia uchaguzi kudai mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi ambapo kwao Uchaguzi Mkuu 2025 ni uwanja wa mapambano.

Alisema wanashiriki uchaguzi kutoa jukwaa kwa vijana wasio na ajira, wakulima na wafanyakazi wanaonyonywa, wananchi waliokandamizwa, kupuuzwa na kuonewa na wanashiriki ili kupigania Taifa la wote, maslahi ya wote.