Serikali yatoa mafunzo kwa wataalamu 2,840 kukabili magonjwa yasiyoambukiza

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 12:42 PM Apr 16 2025
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel.

Serikali imetoa mafunzo kwa jumla ya wataalamu wa afya 2,840, wakiwemo madaktari na wauguzi, ili kuwawezesha kutambua na kushughulikia changamoto zinazohusiana na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo afya ya akili.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Sabu, bungeni jijini Dodoma. Sabu ametaka kujua mpango wa serikali kuhusu kuongeza vituo vya ushauri wa afya ya akili pamoja na programu za uhamasishaji kwa vijana wanaokumbwa na changamoto za afya hiyo.

Akijibu, Dk. Mollel amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za ushauri nasaha na kampeni za uhamasishaji katika ngazi ya jamii. Aliongeza kuwa huduma hizo zinapatikana katika vituo vya afya 701, hospitali zote za rufaa za mikoa pamoja na Hospitali ya Afya ya Akili ya Mirembe.

Dk. Mollel amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za afya ya akili kwa kuimarisha miundombinu na kuongeza wataalamu wa fani hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.