CCM yataja tarehe mpya uchukuaji fomu ubunge, uwakilishi na udiwani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:54 AM Apr 16 2025
news
CCM
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),kimetangaza tarehe mpya ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge,ujumbe wa baraza la wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, kuwa ni Juni 28,mwaka huu.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Aprili 15,2025 na Katibu Mkuu wa CCM,Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi,hatua ya mabadiliko hayo ni baada ya mashauriano na wanachama wake.

"Kwa kuzingatia marekebisho hayo, sasa mchakato huo, utaanza rasmi Juni 28,2025, saa 2:00 asubuhi na kukamilika Julai 2,2025, saa 10:00 jioni, kwa kufuata utaratibu ule ule uliotangazwa kwenye taarifa ya Aprili 10, 2025,"amefafanua.

Ratiba ya awali iliyotangazwa na chama hicho mchakato ulikuwa uanze Mei mosi hadi 15,2025.

"CCM kinapenda kuutangazia umma kwamba baada ya mashauriano na wanachama wake, kutafakari na kupima kwa umakini ushauri huo, kimeamua kufanya marekebisho juu ya ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani."

Katika taarifa ya awali iliyotolewa Aprili 10,2025 na Katibu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, iliwaelekeza wanachama mahali pa kuchukua fomu kwa Tanzania Visiwani na Bara. 

"Utaratibu wa kuchukua na kurejesha fomu za maombi utakuwa kama ifuatavyo: anaogombea nafasi ya Ubunge au Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.
 
 "Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi, kupitia kundi la UWT pamoja na makundi maalumu (NGOS, Wafanyakazi, Wasomi na Walemavu) watachukua fomu na kurudisha kwa Katibu wa UWT wa Mkoa unaohusika.
 
 "Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia jumuiya ya UVCCM watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM Mkoa unaohusika.
 
 "Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia Jumuiya ya Wazazi watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa Wazazi Mkoa unaohusika.
 
 "Waanaogombea nafasi ya Diwani wa Kata (Bara) au Wadi (Zanzibar) watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa Kata/Wadi inayohusika.
 
 "Wanaogombea nafasi ya Udiwani Viti Maalumu vya Wanawake watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UWT wa Wilaya inayohusika."