CAG aeleza hatari barabara za Dar

By Restuta James , Nipashe
Published at 06:02 PM Apr 16 2025
CAG aeleza hatari barabara za Dar.
Picha: Nipashe Digital
CAG aeleza hatari barabara za Dar.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza kuwa miundombinu ya alama za barabarani katika makutano muhimu jijini Dar es Salaam, imepitwa na wakati, hali inayosababisha foleni.

Aidha, erikali imekuwa ikitenga bajeti finyu ya Sh. bilioni 1.8 kwa mwaka, ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Sh. bilioni 200.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni leo Aprili 16, 2025 inaeleza kuwa barabara ya Bagamoyo ina upungufu wa taa kwa asilimia 73, huku mistari ya barabarani iliyofifia na ukosefu wa alama za barabara vikiongeza hatari za ajali.

Inaeleza kuwa upungufu huo umesababisha askari wa usalama barabarani kutumika kudhibiti foleni kwa mikono badala ya taa.

Inasema hali ya ufungaji na matengenezo ya alama za Barabarani zikiwamo taa za kuongoza magari ina kasoro kuanzia kwenye upangaji wa miradi, usimamizi wa mikataba, na matengenezo, inayoathiri usalama wa barabara na ufanisi wa mfumo wa usafirishaji.

“Uharibifu wa vifaa vya barabarani kwenye barabara ya Tabora-Nzega na barabara za Mji wa serikali Dodoma, umesababisha hasara ya Sh. milioni 170.48, huku udhaifu wa hatua za ulinzi ukichangia ongezeko la wizi wa vifaa hivyo,” imefafanua taarifa hiyo.