Katibu wa Kamati Maalum ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amewataka viongozi wa chama hicho ngazi ya mikoa na wilaya kuepuka tabia ya kuwabagua watu kwa misingi ya rangi, dini au kabila, akisisitiza kuwa itikadi ya CCM inatambua kuwa binadamu wote ni sawa.
Mbeto ametoa kauli hiyo leo katika eneo la Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, wakati wa ziara ya Sekretarieti ya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar inayolenga kukagua uhai wa chama katika ngazi ya wilaya kwa maeneo yote ya Zanzibar.
Amesema kuwa sekretarieti imepokea kwa mshangao taarifa za baadhi ya wanachama na viongozi kuanza vitendo vya ubaguzi hasa wakati huu kuelekea zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama.
"Ni jambo la kusikitisha kuona kuna baadhi ya watu wanaanza kujiona wao ni bora zaidi ndani ya chama, na kuwatenga wenzao kwa misingi ya rangi au kabila. Hili siyo sawa kabisa, na siyo sehemu ya misingi ya Chama Cha Mapinduzi," amesema Mbeto.
Ameongeza kuwa CCM ni chama cha wote, na kinaamini katika usawa, mshikamano na heshima kwa kila mtu bila kujali asili yake. Alisisitiza kuwa tabia ya ubaguzi haiwezi kuvumiliwa ndani ya chama na yeyote atakayebainika kuendeleza tabia hiyo atachukuliwa hatua stahiki.
Ziara hiyo ya Sekretarieti ya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar inaendelea katika wilaya mbalimbali kwa lengo la kuimarisha misingi ya chama, kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya chama, na kuhimiza mshikamano miongoni mwa wanachama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED