WIZARA ya Mifugo na Uvuvi, iko kwenye mchakato wa kuanzisha Mamlaka ya Bodi ya Mazao na Miundombinu ya Mifugo, lengo likiwa kusimamia masuala ya sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, Prof Riziki Shemdoe, amesema hayo mjini Morogoro kwenye mkutano wa Nyanda za Malisho Tanzania, uliokwenda sambamba na kongamano la kisayansi la wataalamu wa sekta hiyo.
Amesema bodi hiyo itahusika na masuala yote ya Mazao ya Mifugo na Miundombinu ya Mifugo na kusaidia ustawi wa sekta hiyo, hasa wakati huu ambao wamejikita kuhakikisha ufugaji unakuwa kibiashara.
Aidha akawaasa wafugaji wakiwamo vijana kuanzisha, kumiliki, kuandaa maeneo, kuyaendeleza na kuyawekea miundombinu, kwa ajili ya ufugaji kibiashara katika sekta ya mifugo na kukabiliana na changamoto ya ufugaji wa kuhamahama, unaochangia migogoro ya wakulima na wafugaji.
Kwa kuzingatia hilo akasema wizara hiyo, kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorrow-BBT) imewawezesha vijana 106 kupata mkopo wa shilingi bilioni 934, kwenye vikundi 20 kwa kuwapatia ekari 10 kila mmoja katika ranchi ya Kagoma.
Katibu Mkuu huyo amesema katika kuhakikisha ufugaji unakuwa endelevu na wenye tija ni vyema wafugaji wakamiliki maeneo ya malisho kisheria ya kuendelea na kufuga kibiashara na hiyo itapunguza migogoro ya matumizi ya ardhi na kuleta amani.
Mwenyekiti wa Chama cha Nyanda za Malisho Tanzania (RST), Prof. Ismail Selemani, ameshauri kusimamiwa vyema kwa mustakabali wa maisha ya watanzania kwani zinachangia kuimarisha usalama wa chakula, pato la kaya na kupunguza umaskini.
Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti wa mMifugo Zanzibar, Dk. Talik Saleh Suleiman, amesema kwa sasa wafugaji wa kuku wa Zanzibar, wamekuwa wakiagiza chakula cha kuku kutoka Tanzania bara na hata nje ya nchi, licha ya kuonekana ni changamoto pia ni fursa kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdul Mhite, aliwahimiza watanzania wakiwamo wakulima na wafugaji kufuata sheria za nchi zilizopo hususani Sheria ya Ardhi ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Sura Namba 180 na Mwongozo wa Usimamizi wa Uendelezaji na Upatikanaji wa Maeneo ya Malisho wa Mwaka 2021 katika halmashauri zote nchini.
Anasema kwa sasa serikali imetenga hekta milioni 3.4 kwa ajili ya maeneo ya malisho na kati yake hekta 1.1 yapo kwenye vijiji na 108.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED