LATRA yajivunia mafanikio miaka minne utendaji Rais Samia

By Jane Mathias , Nipashe
Published at 06:33 PM Apr 14 2025
Mkurugenzi wake mkuu, Habibu Suluo
Picha: Mtandao
Mkurugenzi wake mkuu, Habibu Suluo

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imejivunia mafanikio yake kwa kipindi cha miaka minne kwa kusogeza huduma za kwa wananchi na kuwainua kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Mafanikio hayo, yalitangazwa jana na Mkurugenzi wake mkuu, Habibu Suluo katika kikao kazi baina ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa Suluo, mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi hicho cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

“ Kwa maneno uchache, niseme tu kwamba uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia umetujengea mazingira rafiki yenye ushirikishaji wa wadau  kusimamia sekta ya usafiri ardhini. Ninawapongeza pia uongozi mahiri na madhubuti wa wasaidizi wake wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Waziri),  David Kihenzile (Naibu Waziri), Profesa Godius Kahyarara (Katibu Mkuu) na Ludovick Nduhiye (Naibu Katibu Mkuu).

 LATRA ina ofisi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara

Katika kipindi hicho LATRA imesogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa kufungua ofisi katika maeneo ya kimkakati kwenye baadhi halmashari za miji na wilaya nchini. 

Mamla ka hiyo imefungua ofisi 10 katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli Mbezi, Tegeta, na Mbagala (Dar es Salaam). 

 Maeneo mengine ni Makambako (Njombe), Kahama (Shinyanga), Masasi (Mtwara), Ifakara (Morogoro), Korogwe (Tanga), Same (Kilimanjaro) na Nzega (Tabora). 

Amesema mamlaka hiyo inatarajia kuanzisha ofisi nyingine tano katika maeneo ya Gongo la Mboto (Dar es Salaam), Mkuranga (Pwani), Chunya (Mbeya), Mufindi (Iringa), na Nyakanazi (Kagera). 

Amesema LATRA inazingatia dira, dhamira na misingi mikuu iliyojiwekea na kuifuata kwenye utendaji kazi na  majukumu ya kila siku. 

Mafanikio hayo ya LATRA yamepatakana katika kipindi hicho cha kuanzia Februari mwaka 2021 hadi  Machi 2025.

 Ametaja mafanikio hayo kuwa ni utoaji leseni kwa vyombo vya usafiri kwa njia ya barabara.

 “ LATRA ina wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha au kufuta leseni za usafirishaji.
 

 Idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 hadi kufikia 334,859 mwaka 2024/25

 Amelisema kwa mujibu wa takwimu hizo, katika kipindi hicho kiwango cha leseni kilichoongezeka ni 108,658, sawa na asilimia 48.

 “ Hili ongezeko ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne,” amesema.

 Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufikisha huduma karibu na wananchi kwa kufungua ofisi ndogo 10 kwenye maeneo ya kimkakati na hivyo kuwa na ofisi 37 nchi nzima.

Amesema hadi Machi mwaka huu, ofisi hizo zimeonesha mafanikio kwa kufikia wananchi walio mbali na miji mikuu ya mikoa, kuboresha udhibiti wa bodaboda, kutatua migogoro ya wadau, kufikisha elimu kwa wadau na kusogeza ushirikiano na mamlaka kwenye maeneo hayo, ikiwemo Serikali za Mitaa, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mamlaka nyingine. 

Akizungumzia kuhusu usafiri wa mabasi ya mijini, amesema LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa nchini kwa kuanzisha njia mpya 1,007 za daladala jijini Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi.

 Amezitaja njiai zilizorefushwa mijini kwa Dar es Salaam kuwa ni Mbezi Luis – Kisarawe kupitia barabara ya Malamba Mawili, Banana.

 Toangoma – Pugu Stesheni kupitia barabara ya Kilwa, Nyerere, Kivukoni - Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo, Gerezani - Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.

 Buyuni Sokoni - Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi, Bunju Sokoni - Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale, Mbande Kisewe - Gerezani kupitia Barabara ya Kilungule, Chang’ombe na Usalama.

 Mvuti - Machinga Complex na Tabata Segerea, Ngobedi B -Machinga Complex kupitia Nyota Njema na Kitonga - Gerezani kupitia barabara ya Kilwa.

 Kwa upande wa Arusha, LATRA imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi  kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma. 

Njia hizo ni inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Philips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi ‘Fire’ na kurudi kwa Mrombo.  

Katika Jiji la Dodoma ambako ni Makao Makuu ya nchi, imeanzisha njia mpya kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi mapya kutokana na kukua kwa kasi.

Njia hizo ni Machinga Complex - Njedengwa, Machinga Complex - Mpamaa, Machinga Complex - Chidachi, Machinga Complex - Nzuguni, Machinga Complex – Swaswa na Vyeyula - Ilazo

“ Hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex kumesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma, hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” amesema na kuongeza kuwa:
 “Mzunguko huo ni kuanzia Barabara ya Hospitali kupitia Majengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.”

 MWANZA 

Amesema katika jiji hilo, mamlaka hiyo imeanzisha njia ndefu kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi na kukua kwa kasi.

 Njia hiyo ni pamoja na ya kutoka Usagara  – Kisesa kupitia Buzuruga, Ilalila  – Misungwi kupitia Buzuruga na Nyashishi – TX kupitia Kiseke – PPF.

 Nyingine ni Nyashishi  – Kisesa Kona ya Kayenze kupitia Mecco, Nyashishi  – Ilalila  kupitia Buzuruga, Mwanza mjini – Igombe, Mwaloni – Kona ya Kayenze na Mwaloni – Kabusungu.

 USAJI MADEREVA

Kwa upande mwingine, amesema Mamlaka hiyo hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, imesajili madereva 33,778 na taarifa zao kuingizwa kwenye Kanzidata ya Mamlaka hiyo.

 Kati ya madereva hao,  8,172 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe cha Utambuzi wa Dereva.

 Amesema  madereva 4,563 walifaulu mitihani ya LATRA iliyofanyika katika ofisi zake nchini, kati ya 9,191 sawa na ufaulu wa asilimia 49.65  na kupatiwa vyeti vya kuthibitishwa.

 “Matokeo haya yanaashiria maandalizi hafifu kwa madereva, woga wa mitihani unaofanywa kwa kompyuta, upya wa zoezi la kuthibitisha madereva, na kukosekana kwa utaratibu wa kujisomea/kujiendeleza kwa madereva,” amesema Mkurugenzi huyo Mtendaji

 USAFIRI SAA 24

Kuhusu usimamizi wa usafiri wa mabasi usiku na mchana kwa saa 24, alisema  2,323 yalikuwa yamepatiwa ratiba za kutoa huduma za usafiri kwa muda huo.

 Amesema tathmini ya LATRA ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa ruhusa hiyo umebaini wananchi wengi wamefurahishwa kwa kupunguza msongamano wa abiria kwenye vituo vya mabasi na kupunguza tabia ya  madereva kukimbizana barabarani.

 Amesema tathmini ya LATRA inaonesha safari hizo zimepunguza gharama za njiani kwa abiria na kuboresha matumizi ya muda wao kiuchumi, kijamii na kujiongezea vipato.

 TRC, TAZARA 

Kwa njia ya reli nchini, Suluo, amesema ni moja ya eneo linalodhibitiwa na LATRA kwenye usalama wa miundombinu na mabehewa, nauli, viwango vya ubora na ufanisi wa utendaji.

  Amesema katika kipindi hicho, alisema wamemefanya kaguzi 275 katika miundombunu, ishara na mawasiliano, vichwa vya treni na mabehewa na uendeshaji.

  Kati ya hizo, 143 zilikuwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), na 132 Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

 Kuhusu Uanzishwaji wa Huduma za treni za SGR, alisema  LATRA ilikuwa na jukumu la kuthibitisha ubora wa treni kabla ya kuanza kutoa huduma.
“ LATRA iliungana na timu ya wataalamu wa TRC na Wizara ya Uchukuzi kwenda nchi (zilikokuwa zinaundwa) na kukagua na kuthibitisha,” amesema
 

Amesema vichwa vya treni 17, mabehewa ya abiria 56, treni za seti za umeme 10 na mabehewa ya mizigo 264 yalikaguliwa kipindi cha uundwaji katika nchi za Korea, China, Malaysia na Ujerumani.

 Amesema Mamlaka hiyo ilifanya kaguzi za majaribio kwa mabehewa na vichwa hivyo baada ya kuwasili nchini kabla ya kuanza kutoa huduma ili kujirisha usalama wake.

 Amesema katika mwaka wa fedha wa 2023/24, LATRA ilitekeleza jukumu la kisheria kwa kupanga nauli za daraja la uchumi  wakati wa uanzishwaji wa huduma za treni ya kisasa (SGR).

Nauli hizo zilizotangazwa  kwenye Gazeti la Serikali T Juni 14 mwaka jana  Shilingi 31,000 kwa treni ya kawaida na Shilingi 50,000 kwa inayosimama vituo maalum kati ya Dar-es-Salaam na Dodoma.

Nauli kwa mtoto mwenye umri kuanzia miaka minne hadi miaka 12 ni nusu yab hizo na mtoto mwenye umri chini ya miaka minne bure.   

Katika kipindi hicho, LATRA imejenga mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kutoa leseni, usajili wa madereva, malipo na taarifa za udhibiti na kuunganishwa na ya taasisi nyingine za serikali ili kurahisisha uhakiki.

 LATRA ilianzisha Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) unaotumia ‘Satelite’, Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD), Mtandao wa Mawasiliano na Vifaa vya Uhifadhi Data Taarifa  kutuma taarifa za mwenendo mzima wa safari za chombo husika.

 Mafanikio ya usimamizi wa magari kwa mfumo huo hadi kufikia Machi 2023 magari 11,826 yalikuwa yameunganishwa kwenye mfumo huo, kati ya hayo  8,969 yanayotuma taarifa mpaka sasa.
“Wastani wa magari 5,800 yanafanya safari kila siku katika nchi yetu. Idadi hiyo huongezeka katika kipindi cha mwisho wa mwaka na hufikia mpaka magari 6,200 yanayofanya safari kwa siku,” amesema Suluo.

Amesema magari yasiyotuma taarifa, baadhi hayapo barabarani kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na matengenezo ya muda mrefu, ajali, kuungua moto, baadhi kubadili njia  na kuhamia kwenye njia ambazo hazina uhitaji wa VTS.

 Amesema VTS umewezesha utambuzi wa madereva waliothibitishwa wakati wakiwa barabarani na kupewa vitufe vya utambuzi.

 Amesema wa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) na wadau wengine wameunda mfumo jumuishi uliounganishwa na mifumo mingine ya utoaji tiketi kwa abiria nchini.

 Amesema mfumo huo ikiwemo wa TRC na ya tiketi za mabasi unarahisisha ukataji tiketi na kutunza taarifa za abiria. 

 Amesema mfumo huo alioutaka kwa jina la kiganjani, umewekwa katika kituo cha mabasi na treni na kunganishwa na watoa huduma wa tiketi za kielektroniki.

 “Tangu kuanza kuunganisha mifumo ya tiketi za kielektroniki kwenye mfumo huu,  taarifa zetu zinaonesha abiria wa miamala ya tiketi za kielektroniki 13,429,549 ilifanyika. Idadi hii ni sawa na wastani wa abiria 58,137 kwa siku, sawa na wastani wa abiria 1,744,100 kwa mwezi katika kipindi hicho cha siku 231, takriban miezi nane tangu kuanza kutumia mfumo huu,” amesema.

 USAFIRI WA WAYA

 Suluo, amesema rasimu ya kanuni za Udhibiti wa Usafiri wa Waya nchini zilijadiliwa kwenye kikao kilichofanyika Desemba 23, mwaka jana.

 Amesema Bodi ya LATRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inakamilisha mapitio ya muundo wa uongozi na mgawanyo wa majukumu ili kuunda kitengo hicho na kuidhinishwa na Waziri wa Uchukuzi.

Hata hivyo, amesema serikali imeelekeza nguvu zake katika sekta ya utalii kwa usafiri huo kjwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/26.

Vilevile, imejipanga kuhakikisha huduma za usafiri ardhini kwa abiria na mizigo zinakuwa bora, salama na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

LATRA pia inatumia mfumo wa Serikali wa e-Mrejesho kupokea malalamiko, mapendekezo, pongezi au maulizo kwa anwani ya emrejesho.gov.go.tz, e-Mrejesho au kwa simu kwa njia ya msimbo (USSD)  na tovuti www.latra.go.tz na kushughulikia ndani ya siku 21 tangu kuwasilishwa.