MISA TAN: Waandishi mnaogombea wekeni wazi msimamo wenu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:37 PM Apr 14 2025
news
MISA TAN
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), Edwin Soko

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika,Tawi la Tanzania (MISA TAN), imewataka waandishi wa habari kuweka wazi uamuzi wa kugombea kwenye udiwani na ubunge ili kuepusha mgongano kimaslahi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Aprili 14,2025 na Mwenyekiti wa MISA TANZANIA,Edwin Soko, amesema Tanzania inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu Mwezi Oktoba Mwaka huu.

"Uchaguzi huu unatoa haki ya Kikatiba kwa raia wa Tanzania kuchagua viongozi au kuchaguliwa katika nafasi za urais, ubunge, na udiwani. Haki hii inaambatana na masharti kadhaa ya kisheria na kimaadili,"amefafanua.


Soko amesema haki hii inawahusu waandishi wa habari hususan wenye nia ya kugombea, kupigiwa kura, na kuchaguliwa baada ya kutimiza masharti ya uchaguzi yaliyowekwa. 

"Hata hivyo, MISA TAN) inatoa angalizo kwa wanahabari wenye nia ya kutumia haki ya kugombea na kuchaguliwa kuzingatia na kuheshimu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari,"amesema Mwenyekiti huyo.


Aidha, MISA TAN imewahimiza wanahabari wenye nia au waliofanya uamuzi wa kugombea katika uchaguzi ujao kutangaza nia au uamuzi wao wa kugombea katika uchaguzi mkuu ujao kupitia vyombo vyao na taasisi zao za kihabari, ili taratibu za kimaadili zifuatwe.

Soko amesema kwa waandishi wa habari watakaotangaza nia wanatakiwa kutojishughulisha na majukumu ya uandishi wa habari za uchaguzi ili kuepuka mgongano wa kimaslahi na upendeleo katika kuhabarisha umma

"Hatua hii inalenga kuimarisha weledi na imani ya wananchi na wadau kwa vyombo vya habari katika kuripoti masuala ya uchaguzi,"amesema.


"MISA TAN itaendelea kuhimiza kulindwa kwa uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa kama msingi wa kuimarisha demokrasia, uwazi, na utawala bora hapa nchini,"amesema.