Serikali imechukua hatua madhubuti kusaidia matibabu ya watu wenye ualbino kwa kuanzisha vituo maalum vya uchunguzi na matibabu ya saratani ya ngozi katika hospitali mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa leo, Aprili 14, bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Taya, aliyehoji kuhusu utaratibu wa serikali katika kusaidia matibabu ya ngozi kwa watu wenye ualbino, hasa kutokana na kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani ya ngozi.
Dk. Mollel amesema serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ualbino na tayari imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuanzisha vituo hivyo maalum ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Amesema hatua nyingine ni kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kinga, hasa mafuta maalum ya kujikinga na jua, ambayo sasa yamejumuishwa kwenye bidhaa za afya zinazoagizwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Aidha, amesema serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu Wenye Ualbino (MTHUWWU) unaolenga kuboresha huduma za afya, elimu, na ulinzi dhidi ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED