NEMC, TK Movement wazindua jukwaa rasmi la mazingira

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 06:46 PM Apr 14 2025
Naibu Mratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya TK Movement inayojihusisha na shughuli za utoaji elimu ya utunzaji mazingira Halima Rajabu (watano kushoto), Mkurugenzi wa Shirika la Africa Guarantee Fungi.
Picha: Maulid Mmbaga
Naibu Mratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya TK Movement inayojihusisha na shughuli za utoaji elimu ya utunzaji mazingira Halima Rajabu (watano kushoto), Mkurugenzi wa Shirika la Africa Guarantee Fungi.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na taasisi isiyo ya kiserikali kuzindua Jukwaa la Uchumi wa Kijani ambalo litatumika mahususi katika utoaji elimu na kuwakutanisha wadau wote wa mazingira kujadili masuala mbalimbali ikiwemo changamoto za kimazingira na kuzipatia suluhu.

Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi wa Kijani linaloratibiwa na Taasisi ya TK Movement, Ofisa Mazingira wa NEMC, Grace Tupa, alisema kipitia jukwa hilo watakuwa bega kwa bega katika utoaji wa elimu na kuhamasisha wanafikia malengo ya uchumi wa kijani hasa katika kuzitumi taka kama fursa ya kujitengenezea kipato.

Alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya NEMC katika kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelewesha juu ya kutumia taka kama fursa na kujua ni namna gani ya kutenga taka hatarishi na ambazo zinaweza kutumika tena kutengeneza vitu vinavyoweza kuwaingizia kipato.

“Wananchi watumie vizuri fursa hii kwasababu ujio wa programu hii watapata kuelewa maana ya uchumi wa kijani na ni namna gani ya kutenganisha taka na hatimaye kuzibeba kama taka fursa ya kujipatia kipato.


“NEMC tunaipogeza TK Movement kwasababa wameenda kuigusa jamii moja kwa moja na kupitia Jukwaa la Uchumi wa Kijani wananchi watapata kujua jinsi gani tunatakiwa kuhifadhi mazingira kwa afya zetu sote,” alisema Grace.

1

Pia alitoa wito kwa wengine kuunga mkono jitihada hizo ili kulifanya jambo hilo la utoaji elimu ya utunzaji mazingira kuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae.

“Uchumi wa kijani unatokana na taka zinazotuzunguka katika mazingira yetu ambazo tunaweza kuzihifadhi vizuri na kuzitumia katika kujiingizia kipato. Tunatamani elimu hii iwafikie watanzania wote waelewe, na tuko tayari kushirikiana na wadau wote kupeleka elimu kwa jamii,” alisema Grace.


Mratibu wa TK Movement Dar es Salaam, Herman Kajiru, alisema kuanzishwa kwa Jukwaa la Uchumi wa Kijani walidhamiria kujenga eneo moja litakalowakutanisha wadau wote wa mazingira na kujadili masuala mbalimbali pamoja na changamoto za kimazingira na kuzipatia suluhu.

“Ukiangalia kwa sasa kuna vitu vingi vimeanzishwa lakini havijatambulishwa rasmi kwamba ni uchumi wa kijani, kumeanzisha matumizi ya sola hizo zote ni nishati safi, kuna wanaosafisha fukwe na kuokota makopo hizo zote ni ‘elements’ za uchumi wa kijani kwasababu zinaleta manufaa kwa mazingira.

2

“Watu waone kwamba kupitia uchumi wa kijani tunaweza kupata fursa kama shughuli za kiuchumi, na TK Movemen tunaona baada ya uzinduzi wa jukwaa hili tunachokiona ni jamii yenye uelewa juu ya utunzaji mazingira, na kutakuwa na mafunzo mbalimbali yatakayofanyika mara kwa mara kuanzia sasa,” alisema Kajiru.


Naye, Naibu Mratibu wa TK Movement Mkoa wa Dar es Salaam, Halima Rajabu, alisema wamekuja na programu hiyo kwa lengo mahususi la kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika suala zima la utunzaji mazingira ambalo limepewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa nchini.

Mkurugenzi wa Shirika la African Guarantee Fund, inayojihusiha na uwezeshaji wa dhamana kwa benki na taasisi zinazojihusisha na shughuli za utunzaji mazingira, Patric Lumumba, alisema wameunga mkono suala hilo kwasababu linaenda kuwagusa wananchi hasa wanawake.

“Suala la umuhimu kwetu ni kuona mazingira yanatunzwa na kuwa ya kijani kwaajili ya manufaa ya leo na kesho, ndio maana tumeshawishika kushiriki katika programu ya Ilala ya Kijani,” alisema Lumumba.