Jafo asikia kilio cha mabinti sekondari Jokate Mwegelo

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:18 PM Apr 14 2025
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo
Picha: Julieth Mkireri
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo, amemwagiza Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, kukutana na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kwa ajili ya kutafuta chumba maalumu cha zahanati na mtaalamu wa afya katika shule ya Sekondari ya Wasichana Jokate Mwegelo.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, ametoa maagizo hayo, baada ya kusomwa kwa risala ya wanafunzi wa shule hiyo, kwenye mahafali ya kidato cha sita, ambao waliomba kuwa na jengo la kupumzikia wagonjwa na mtaalamu wa afya kuwapatia wa matibabu pale inapohitajika.

Jafo asikia kilio cha mabinti sekondari Jokate Mwegelo
Akizungumza katika mahafali hayo, Jafo amesema kuwa na mtaalamu wa afya pamoja na zahanati katika shule hiyo, ni muhimu itawasaidia wanafunzi kupatiwa matibabu karibu badala ya sasa wanatumia zahanati ya kijiji.

Kadhalika akizungumzia kuhusiana na miundombinu ya shule hiyo Dk. Jafo amesema, serikali inakwenda kutatua tatizo la uhaba wa nyumba za walimu pamoja na maabara za sayansi kwenye shule hiyo, ambayo lengo la kuanzishwa kwake ni kutokomeza ziro wilaya ya Kisarawe.

Jafo asikia kilio cha mabinti sekondari Jokate Mwegelo
"Tunataka Jokate Mwegelo iwe kati ya shule tano bora kitaifana tutahakikisha inakuwa kipaumbele katika shule za Kisarawe, changamoto zilizopo tunakwenda kuzitafutia ufumbuzi na tayari nyingine tumeanza kuzitatua," amesema 

Mkuu wa shule hiyo, Mariamu Mpunga, amesema kikwazo kinachoikabili shule hiyo ni pamoja na uhaba wa nyumba za walimu sambamba na maabara za sayansi ambazo zimekuwa chanzo cha kushuka ufaulu wa wanafunzi.

Alimwomba Waziri huyo kusimamia utatuzi wa vikwazo, ili shule hiyo kuendelea kuwa kinara kwenye mitihani ya kitaifa katika mkondo wa sayansi na masomo mengine.

Awali akisoma risala ya shule hiyo, kwa niaba ya wanafunzi wengine, Theresia Mbwambo, amesema shule inakabiliwa na kikwazo cha upungufu wa walimu , nyumba za walimu uhaba wa maabara za sayansi, ukosefu wa uzio, gari la wanafunzi na sehemu ya kupumzikia wagonjwa 

Shule ya Sekondari ya Wasichana Jokate Mwegelo, ilianzishwa mwaka 2021 ikiwa na lengo la kutokomeza zero katika Wilaya ya Kisarawe na hadi sasa ina wanafunzi 1,008 huku wahitimu wa kidato cha sita wanatarajiwa kufanya mitihani hivi karibuni, wakiwa 270.