WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali itaendelea kutoa fedha kufanikisha utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ili ziwe endelevu.
Kadhalika lengo ni kufikia malengo yaliyokusudiwa hasa ya kukuza lugha ya kiswahili nchini na duniani kwa ujumla.
Ulega ameyasema hayo leo, wakati alipomwakilisha Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo zinazoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.
Amesema utoaji wa tuzo hiyo, ni ishara ya kuendelea kuenzi utamaduni wa hayati Nyerere, Afrika na duniani, hivyo anaitaka TET kuhakikisha tuzo hiyo inakuwa endelevu, ili kufanikisha malengo yale yaliyokusudiwa.
“Utoaji wa tuzo za uandishi bunifu katika lugha ya Kiswahili, ni ishara ya kuedelea kuikuza lugha hii na utamduni wake Afrika na duniani kwa ujumla.
“Hata hivyo maandiko bunifu yenye tija ni yale yanayoisaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo kijamii, kiuchumi, kisayansi na tekonolojia, nitoe wito kwa watanzania wezangu kujitokeza kushiriki kwa kuwasilisha miswada yao, ili kushindania tuzo hii.
“Niwapongeze sana washindi wa mwaka huu na wote waliowasilisha miswada yao na wale ambao hawatakuwa washindi niwaombe wasikate tamaa ya kuwania tuzo hii, muhimu.
“Meendelee kujifunza muandike nini na kwa wakati gani, serikali yetu itaendelea kutoa fedha za kufanikisha utoaji wa tuzo hii, ili iwezeshe kufanikisha malengo makuu,” amesema Ulega.
Ameongeza kwa kuiomba TET ambao ndio waratibu, kuhakikisha tuzo hiyo inatolewa kila mwaka, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa pia ametoa wito kwa watanzania, kuendelea kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kazi zao ili kushiriki tuzo hiyo.
“Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, aliendeleza lugha ya kiswahili kwa kuwa mwandishi bunifu wa mashairi na riwaya, hivyo jambo hili la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ni la heshima kwani linamuenzi Mwalimu pamoja na kazi zake,” amesema Ulega.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba, amesisitiza kuwa serikali itagharamia uchapishaji na usambazaji shuleni wa nakala za vitabu vitakavyoshinda tuzo hiyo katika nyanja ya riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthilia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere, Prof. Penina Mlama, amesema kamati imefurahi kuona mwitikio wa waandishi bunifu kushiriki tuzo hizo umekuwa mkubwa na jumla ya kazi zilizopokelewa mwaka huu ni 282 ikilinganishwa na 209 mwaka jana na 283 ya mwaka wa kwanza zilipoanza tuzo hizo.
Prof. Mlama amesema kwamba kati ya miswada 282 iliyowasilishwa mwaka huu ya ushairi ilikuwa 114, riwaya 46, hadhiti za watoto 77 na tamthilia ni 45.
“Hata hivyo kwa mwaka huu jumla ya miswada iliyotimiza vigezo vilivyowekwa ilikuwa ni 205 kati ya 282, naendelea kuwasihi sana waandishi bunifu kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
“Kuepuka kuwasilisha kazi ambazo hazijazingatia vigezo, washiriki wa mwaka huu wametoka katika mikoa yote ya Tanzania na miswada minne imetoka kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi,” amesema Mlama.
Vile vile, amesema kati ya washiriki wote wa tuzo hiyo wanawake walikuwa 88 sawa na asilimia 32 na kwamba hilo ni ongezeko kutoka washiriki 62 mwaka jana na kwamba mwaka huu wanaume ni 194 ikilinganishwa na 155 wa mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Maktaba ya Taifa, Dk. Mboni Ruzegea, amesema maktaba inatambua na kuthamini kazi bunifu zinazofanywa na waandishi bunifu wanaotumia lugha ya Kiswahili, ambayo ni urithi hai unaotakiwa kutunzwa, kulindwa na kusambazwa katika maktaba kwa ajili ya manufaa ya kizazi kijacho.
Amesema wao kama Maktaba ya Taifa wanalo jukumu la kuhakikisha wanasajili kazi za waandishi bunifu na kuwapatia namba maalumu ya vitambulisho ambayo inatolewa na maktaba ya taifa pekee na kusambaza kazi zao.
Mhadhiri, Mwandishi wa vitabu na mchoraji maarufu kutoka Chuo Kikuu cha Sultan Quaboos cha nchini Oman, Prof. Ibrahim Noor Shariff, amesema ubunifu katika lugha ya Kiswahili, umeenea katika nchi za Afrika Mashariki na kumekuwa na mwamko mkubwa wa kuenea kwa lugha hiyo duniani.
“Mtu akipata fursa ya kusafiri na kufika hadi Manga (jina la zamani la Omani) ukatembea majabarini na katika masoko ukataka kumsengenya mtu hapa utaaibika maana kiswahili kimekuwa kwa kasi na kinasemwa na wengi huko,” amesema Shariff.
Amesistiza kuwa lugha ya kiswahili imekuwa tunu barani Afrika kwani kinazungumzwa na wakazi wengi katika nchi za bara hilo.
Washindi wa kwanza wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu 2025 kutoka vipengele vinne ambavyo ni Ushairi, Riwaya, Tamthilia na Vitabu vya Watoto wamepokea mfano wa hundi ya Sh. milioni 10 kwa kila mmoja.
Washindi hao ambao ni Tyatawelu Kingu, Maundu Mwingizi, Hussein Abdallah na Tune Salim walikabidhiwa mfano wa hundi hizo za Sh. milioni 10, ngao, cheti pamoja na miswada yao kuchapishwa kwa gharama ya serikali na kusambazwa katika shule mbalimbali pamoja na kuwekwa kwenye Maktaba za Taifa.
Tuzo hiyo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, walikabidhiwa na Waziri Ulega, kwa niaba ya Makamu wa Rais Dk. Mpango.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED