Msigwa:Tanzania iko salama mikononi mwa Rais Samia

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:27 PM Apr 11 2025
Mchungaji Peter Msigwa
Picha:Mtandao
Mchungaji Peter Msigwa

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Peter Msigwa, amesema Tanzania iko salama kwenye mikono ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo leo Aprili 11,2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara unaofanyika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya siku 10 ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA  Amos Makalla, akizungukia mikoa miwili Lindi na Mtwara.

Amesema vyama vinapaswa kutengeneza siasa inayohusu uchumi kutoka kwenye uduni hadi ubora, ambapo CCM ndicho inachokifanya.

“Nilikuwa kipofu kama yule Sauli na sasa naona nimeamua kujiunga CCM. Vyama vingine vipo kwaajili ya kupinga na si kujali maslahi ya Watanzania, hoja zao ni za namna ya kuingia madarakani na siyo hoja ya kumkwamua mwananchi na suala la korosho, elimu, afya,” amesema.

Mwanachama CCM, Amidu Bobal, amesema Liwale ilikuwa ya Chama cha Wananchi (CUF) wakiongoza halmashauri, lakini  yamemshinda na kuamua kurejea chama tawala kwa sababu ya maendeleo yanayofanyika.

“Liwale kukishafanyika fujo nyumba 28 zikachomwa na barabara zikafungwa huko tumeshatoka, ninawaambia njia sahihi ni CCM na tuna jemedari mahiri Rais Samia. Liwale inategemea  korosho, ufuta na misitu na Rais Samia ameweka sawa,” anasema.

Mwanachama CCM, Abdul Kambaya, anasema dunia nzima hakuna chama kinachoweza kuwafikisha peponi au motoni, bali watakwenda kwa matendo.

“Chama kinachoweza kutatua matatizo ya Watanzania ni CCM pekee, mkitaka maendeleo njooni CCM kiungeni mkono ili kuendeleza tulikoishia,” anasema.