Chama cha ACT Wazalendo kinapenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa kimezindua rasmi programu ya mafunzo kwa majimbo 189 kutoka katika kanda 8 za kichama, ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hiyo muhimu.
Mafunzo hayo yalizinduliwa rasmi tarehe 12 Aprili 2025 na viongozi wakuu wa chama wakiongozwa na Kiongozi wa Chama, Doroth Semu, pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita; Katibu Mkuu, Ado Shaibu; Naibu Katibu Mkuu Bara, Ester Thomas; na Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mafunzo hayo ni pamoja na kufafanua kwa kina maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa, hususan kuhusu utekelezaji wa Oparesheni Linda Demokrasia – mkakati madhubuti wa chama unaolenga kuhakikisha chaguzi nchini zinakuwa huru, za haki, na zinazokubalika na wananchi wote.
ACT Wazalendo inaendelea kutekeleza maagizo ya Halmashauri Kuu ya Chama iliyoketi tarehe 23 Februari 2025, ambayo ilisisitiza umuhimu wa kufika kila kona ya nchi kwa ajili ya kuwaeleza wanachama, viongozi na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kulinda demokrasia, ili taifa letu lirejeshe imani na thamani ya kura ya mwananchi.
Awamu ya pili ya mafunzo hayo itaendelea kwa lengo mahsusi la kuhakikisha majimbo yote 214 ya Bara yanafikiwa na programu hii ya mafunzo ya kimkakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED