Hadi hivi sasa rekodi ya Guinness inamtambua Rumeysa Gelgi, aliyezaliwa tarehe 1 Januari 1997, kuwa mwanamke mrefu zaidi aliye hai tangu mwaka 2021.
Gelgi ambaye ni mtaalamu wa mtandao kutoka Uturuki anajulikana kwa kuwa na rekodi hiyo ya Guinness World Record, ingawa kuna wanawake wengine ambao hawajathibitishwa na Guinness wanaojulikana kuwa mrefu zaidi.
Gelgi ana urefu wa sentimita 215.16 (mita 2.15 au futi 7.0.71) na uzito wa kilo 90 anaishi katika mkoa wa Karabük, Uturuki.
Urefu wake unatokana na ugonjwa wa Weaver, hali nadra ambayo inasababisha ukuaji wa haraka pamoja na matatizo mengine ya kiafya.
Ugonjwa huu unaelezwa kuwapata wanaume mara tatu zaidi kuliko wanawake.
Kutokana na hali yake, mara nyingi hutumia kiti cha magurudumu kwa usafiri, ingawa anaweza kutembea kwa muda mfupi kwa kutumia msaidizi wa kutembea.
Miongoni mwa changamoto zake, hawezi kuketi kwenye viti vyenye urefu chini ya sentimita 50-55.
Septemba 28, 2022, Gelgi alifanya safari ya ndege kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
Chakushangaza Shirika la ndege la Turkish Airlines lililazimika kuweka godoro juu ya safu sita za viti kwenye ndege yao ili kumwezesha kusafiri kutoka Istanbul, Uturuki, hadi San Francisco, California, Marekani.
Tukio hili lilivutia waandishi wa habari na kuonyeshwa katika filamu ya dokumentari ya Guinness World Records iitwayo "Rumeysa: Walking Tall."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED