WAZIRI wa Malisili na Utalii, Angellah Kairuki, amesema maboresho yaliyofanywa na serikali katika sekta ya utalii yamechangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii wa nje ya nchi na ndani wanaotembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo wakati akizindua maonesho ya Karibu Kili Fair (KKF) katika msimu wa tisa ambayo yameshirikisha wanunuzi zaidi ya 600 wa bidhaa mbalimbali za utalii kutoka nchi zaidi ya 42 duniani na wadau wa utalii 468 kutoka nchi 37.
Amesema mazingira bora ya biashara kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi yamekuwa na tija kubwa katika sekta ya utalii.
"Tumeona idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wakiongezeka kila siku.Nataka niwahakikishie kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hii muhimu kwa taifa,"amesema.
Waziri Kairuki amesema maonesho hayo ya kimataifa Karibu Kili Fair yana tija kubwa kwa kuwa yanawakutanisha watoa huduma za utalii nchini na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali za utalii ikwemo safari na hoteli
Naye Mkurugenzi wa maonyesho hayo, Dominic Shoo, amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Arusha na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Shoo amesema waoneshaji wa bidhaa mbalimbali kwa msimu huu wa tisa ni zaidi ya 450 kutoka Tanzania, Ghana, Burundi, Cameroon na Afrika Kusini huku makampuni zaidi ya 700 kutoka nchi zaidi ya 40 wakishiriki kwenye msimu huu.
Amesema maonyesho hayo yatadumu kwa siku tatu mfululizo yanatoa fursa ya kiuchumi kwa kutoa fursa kwenye sekta ya kilimo, usafiri, utalii na kubadilishana uzoefu kutokana na wingi wa wageni na wadau wa utalii wanaotarajiwa kuhudhuria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED