Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyama vya siasa na Serikali kesho wanatarajiwa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na vyombo vya habari mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhan amesema chama cha siasa ambacho hakitasaini maadili hayo hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Kailima amesema maadili hayo yameandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Amesema kifungu hicho kinaelekeza kuwa kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.
Ameongeza kuwa tayari maandalizi yote muhimu yameshafanyika na mawasiliano yameshafanyika baina ya Tume, Serikali na vyama vya siasa na kwamba kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo za maadili kesho.
Amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku moja tu na kwamba baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni hizo za maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED