Kliniki ya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya inatarajiwa kujengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni jitihada za kutoa msaada wa kitabibu kwa waathirika wa dawa hizo na kuwasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida ya maisha.
Hayo yamebainishwa leo, Juni 19, 2025, katika kikao cha wadau wa huduma za afya kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT) kilichofanyika mkoani Shinyanga, kikao ambacho kiliandaliwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ajili ya kujadili eneo mahsusi litakalojengwa kliniki hiyo.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa THPS, George Anatory, amesema ujenzi wa kliniki hiyo unatarajiwa kuchukua miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2025, kwa ufadhili wa taasisi moja ya kifedha kwa gharama ya Shilingi milioni 134.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni hatua kubwa ya mabadiliko kwa mkoa wa Shinyanga, hasa kwa watu wanaokabiliwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, kwani watapata tiba, ushauri nasaha na huduma za kurekebisha tabia.
“Kliniki hii ya MAT itakuwa ya kipekee mkoani Shinyanga, na itatoa huduma muhimu za afya kwa waraibu wa dawa za kulevya,” amesema Anatory.
Naye Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Erasmus Mndeme, amepongeza uanzishwaji wa kliniki hiyo, akieleza kuwa huduma hizo zinaendelea kupanuliwa nchini, huku akitaja dawa inayotumika katika tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya kuwa ni Methadone, hasa kwa wanaotumia Heroini.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile, akiendesha majadiliano ya wadau kuhusu eneo la ujenzi, alitaja maeneo yaliyopendekezwa kuwa ni Kituo cha Afya Kambarage, Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Hata hivyo, baada ya majadiliano hayo, wadau walikubaliana kwa pamoja kuwa kliniki hiyo ijengwe katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED