Mwenyekiti TAMWA aaga, asisitiza usawa habari za uchaguzi

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 03:45 PM Jun 19 2025
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe (wa pili kushoto), akizungumza alipotembelea ofisi za Kampuni ya The Guardian Ltd (TGL), wachapishaji wa magazeti ya The Guardian na Nipashe, Mikocheni Viwandani.
PICHA: JOHN BADI
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe (wa pili kushoto), akizungumza alipotembelea ofisi za Kampuni ya The Guardian Ltd (TGL), wachapishaji wa magazeti ya The Guardian na Nipashe, Mikocheni Viwandani.

Vyombo vya habari nchini vimeshauriwa kuzingatia uwiano wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi maalum wakiwamo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kuripoti habari za uchaguzi, badala ya kuzipa nafasi sauti za wanasiasa pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 19, 2025 na Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe, wakati wa ziara maalum katika makao makuu ya The Guardian Limited, akiwa katika hatua za kuhitimisha kipindi chake cha uongozi wa awamu ya pili ndani ya chama hicho.

Amesema licha ya hatua chanya zilizopigwa katika sekta ya habari, bado kuna changamoto katika kuripoti usawa wa kijinsia hasa wakati wa uchaguzi na mara nyingi sauti za makundi maalum hukosa uwakilishi wa kutosha.

“Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kujenga jamii jumuishi. Tuwe na taarifa zinazowakilisha kila kundi, sio tu wanasiasa,” amesisitiza Shebe.

Akipongeza The Guardian, Shebe amesema:

 “Nawapongeza kwa kushiriki Tuzo za Samia Kalamu Award na hata kushinda, ni ushahidi kuwa mna waandishi wenye weledi na uongozi bora. Hii ni kazi ya mfano. Wapo baadhi ya vyombo havikuwasilisha kazi, lakini ninyi mlifanya vizuri na kazi zenu zilionesha kujibu mahitaji ya jamii.”

Shebe ameongeza kuwa TAMWA imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kwenye masuala ya jinsia, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake kuingia katika nafasi za uongozi, uhariri, na hata kazi za upigaji picha.

“Nimetembelea ofisi hii kuwashukuru kwa ushirikiano wakati wa uongozi wangu. Ninatambua pia uwapo wa wanachama hai wa TAMWA hapa ndani. Nawashukuru sana. Sasa naelekea kumaliza muda wangu na nitaendelea kuwa mshauri,” amesema Shebe.

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe, amebainisha kuwa chombo hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye kazi zao za kihabari.

“Tumekuwa tukizingatia uwiano sahihi katika habari zetu, hasa kipindi cha uchaguzi. Mwaka jana tulitambuliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan Research Institute, kwenye utafiti wao kuwa Nipashe ni gazeti namba moja kwa Tanzania na wa nne Afrika Mashariki kwa kuandika habari za usawa wa kijinsia,” amesema Bandawe.

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la The Guardian, Wallace Mauggo, amethibitisha kuwa hakuna ubaguzi wa kijinsia ndani ya gazeti hilo tangu aanze kazi mwaka 1994. “Toka nimeanza hapa, tumekuwa tukiheshimu na kuzingatia usawa wa kijinsia katika kila hatua ya uhariri na uchapishaji wa habari. Hii ni sehemu ya utamaduni wetu wa kazi,” amesema Mauggo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa The Guardian Limited, Jackson Paulo, ameishukuru TAMWA kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika tasnia ya habari na kupongeza uongozi wa Shebe kwa kushirikiana vizuri na vyombo vya habari.

 “Tuzo za Samia Kalamu mliotutunuku ni heshima kubwa kwetu. Tutaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunasimamia usawa na taaluma bora ya habari,” amesema Jackson.