Wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha mifumo ya kidijitali kwani imerahisisha upatikanaji wa huduma.
Pongezi za wanachama hao zimetolewa mbele ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, PSSSF, Paul Kijazi, wakati akiongoza timu ya wataalamu wa PSSSF kutembelea banda kwa banda ili kupata maoni ya wanachama kuhusu utendaji wa mfuko lakini pia kuwaunganisha na PSSSF Kidijitali.
"Suala la mifumo ya TEHAMA, Mhe. Rais Samia, amelipa kipaumbele, zamani ili niweze kujua mtiririko wa michango yangu lazima nisafiri ili kuifuata ofisi ya PSSSF kupata taarifa hizo, lakini hivi sasa mimi mwenyewe nikiwa na simu yangu kwenye kituo changu cha kazi, naweza kupata taarifa zote zinazohusiana na uanachama wangu.” amepongeza Beatrice Augustine, Mwanachama wa PSSSF.
Kwa sasa huduma zenu ni nzuri sana, zamani mlolongo ulikuwa mrefu, lakini hivi sasa mambo yote online, ameongeza Mwanachama mwingine Hellen Agrey.
Mwanachama mwingine amesema, kutokana na kuimarika kwa mifumo ya TEHAMA, amekuwa akifurahia maisha kutokana na kupata huduma kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala PSSSF, Paul Kijazi amesema PSSSF ina utaratibu wa kuwafikia wateja (wanachama) na sio tu wakati wa maonesho bali hata katika utoaji wa kawaida wa huduma huwa wanawatembelea wanachama.
“Hivyo tunayatumia maonesho haya kuwatembelea wanachama wetu ili kupata maoni na tunaenda sambamba na kauli mbiu ya maonesho ya kuhimiza matumizi ya kidijitali.” amefafanua Kijazi
Kuhusu TEHAMA, amesema asilimia 90 ya huduma zote za PSSSF zinapatikana kwa njia ya kidijitali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED