Ikiwa ni takriban wiki moja tangu Mahakama kuzuia shughuli za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA), chama hicho sasa kimegeukia katika shughuli za kijamii ili kuendelea na kampeni yake ya ‘no reforms no election’.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche tayari ameshatoa maelekezo kwa viongozi wa chama hicho nchi nzima kushiriki katika shughuli za kijamii kama vile kupanda miti, kuona wagonjwa na kutembelea watoto yatima.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo hatua hiyo itaendeleza juhudi za chama hicho kupambania mabadiliko ya uchaguzi wanayoyataka ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki, huku ikijiepusha kutumia rasilimali za chama kama ilivyoelekezwa na Mahakama.
“Sisi tunataka kura iwe na nguvu ili Serikali iwajibike kwa wananchi ,wananchi ndio wawe na uwezo wa kusema kama Katiba inavyosema, ndiyo tunachojaribu kusema wananchi waelewe ili watuunge mkono”
“Kuna watu wanasema watapoteza ndoto zao za kuwa wabunge kuwa madiwani sasa watu kama hao wananchi watawapiganiaje mpaka kufa kama wao hawana uwezo wa kukubali kupoteza ubunge, udiwani au hata Urais kwa ajili ya kupigania wananchi?”-John Heche.
Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam wiki iliyopita ilizuia kwa muda shughuli za kisiasa za CHADEMA na kwa mujibu wa hati ya malalamiko, walalamikaji wanadai kuna mgawanyo usio sawa wa rasilimali za kifedha kati ya Bara na Zanzibar ndani ya chama hicho.
Aidha, wamelalamikia pia kuwepo kwa ubaguzi wa kijinsia, udini, na matamko yanayodaiwa kuwa na nia ya kuvuruga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa baada ya wakili wa Chadema, Jebra Kambole, kujiondoa katika kuendelea kuisimamia kesi hiyo mapema Jumanne, akilalamikia kuwa hoja za mawakili hazikusikilizwa ipasavyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED