Aliyekuwa Mbunge wa Mtwara Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Hatua hiyo imechukuliwa leo, Juni 19, 2025, katika kongamano maalum la kisiasa lililofanyika kwenye Ukumbi wa Kanisa la Pentekoste mjini Mtwara, na kuhudhuriwa na viongozi wa ACT Wazalendo, wanachama na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Katika tukio hilo, Nachuma alikabidhiwa kadi ya uanachama na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, na kueleza kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina kuhusu mwelekeo wa siasa nchini.
“Nimeamua kujiunga na ACT Wazalendo kwa sababu ni chama kinachojikita katika misingi ya uwajibikaji, siasa safi na uchumi jumuishi. Ninaamini kupitia chama hiki, tunaweza kuleta mageuzi ya kweli kwa wananchi,” amesema Nachuma.
Mbali na yeye, Nachuma amesema ameambatana na wanachama wapatao 2,600 kutoka CUF, hasa kutoka maeneo ya Mtwara na kusini mwa Tanzania, ambao pia wamehamia ACT Wazalendo.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amesema uamuzi wa Nachuma kujiunga na chama hicho ni ishara ya kuimarika kwa chama na kuongeza uzoefu katika harakati zake za kisiasa. “Tunamtambua kama kiongozi mwenye historia katika siasa za upinzani na tunaamini atatoa mchango mkubwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” amesema.
Aidha, baadhi ya wachambuzi wa siasa waliozungumza na gazeti hili wamesema hatua hiyo inaweza kuathiri nguvu ya CUF katika ukanda wa kusini, ambapo Nachuma ameendelea kuwa na ushawishi wa kisiasa tangu alipokuwa mbunge.
Tukio hilo limekuja wakati vyama vya siasa nchini vikiendelea na maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambapo vyama vingi vinajipanga kuongeza ushindani, hasa katika maeneo yaliyoonesha mabadiliko ya kisiasa katika chaguzi zilizopita.
Kwa mujibu wa Nachuma, sasa atajielekeza katika kushiriki kikamilifu kwenye mikakati ya kisiasa ya ACT Wazalendo, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika kampeni za kuhamasisha wananchi kuhusu sera za chama hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED