Jaji kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki aliyeachiwa huru

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 02:31 PM Jun 20 2025
Jaji kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki aliyeachiwa huru
Picha: Mpigapicha Wetu
Jaji kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki aliyeachiwa huru

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi, anatarajiwa kusikiliza maombi ya kuongeza muda wa kukata rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki, Ibrahim Masahi, aliyekuwa ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni. Kesi hiyo itasikilizwa Julai 1, 2025.

Awali, Masahi alihukumiwa Januari 11, 2023 kwa tuhuma za kumpiga kwa nyundo Deogratus Minja akiwa eneo la Mbezi Msakuzi, ndani ya Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, na kumsababishia majeraha makubwa mwilini.

Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni ilimuachia huru Masahi baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, ikibaini kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote.

Kutokana na hukumu hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga maamuzi hayo, ukieleza kuwa Hakimu Mkazi Amos Rweikiza hakutenda haki kwa sababu mshtakiwa hakueleza namna alivyomtambua mshitakiwa usiku wa tukio.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kuwa uliweza kuthibitisha shtaka hilo kwa ushahidi wa shahidi wao aliyeeleza jinsi alivyomtambua Masahi kwa msaada wa mwanga wa taa uliokuwepo eneo la tukio hilo.

Kwa upande mwingine, mjibu wa maombi (Masahi) kupitia kwa wakili wake, Nehemiah Nkoko, amewasilisha majibu ya maombi hayo kwa njia ya kiapo kinzani dhidi ya hoja za upande wa mashtaka (Jamhuri).

Katika ushahidi wake, Minja alidai kuwa siku ya tukio, saa mbili na nusu usiku, alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake, Masahi. Alipofika hapo, alikutana na kijana wa jirani huyo ambaye alianza kuzungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa, lugha ambayo Minja hakuiweza.

Minja amedai kuwa ghafla kijana huyo alikwenda mbele yake na kumzuia asipite. Geti likafunguliwa na Masahi akatoka nje, akimuuliza Minja ni nani na kwanini amekwenda kumshtaki kwa Serikali za Mitaa. Minja hakujibu, ndipo kijana wa mjibu maombi alipompiga ngumi.

“Alipoinua shati lake juu akatoa nyundo akanipiga nayo kichwani. Baada ya kupata maumivu makali nilianza kukimbia huku nikipiga kelele kuomba msaada,” alidai Minja.