Katika tukio la kitaifa la kisayansi, Prof. Razack Bakari Lokina, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ametoa wito wa kuharakishwa kwa utekelezaji wa awali (piloting) wa mfumo wa AkiliCheck katika Kituo cha Afya cha UDOM.
Wito huu umetolewa wakati ambapo timu ya mradi wa AI4MH inajiandaa kusambaza mfumo huo kwenye vituo vingine vya afya ndani na nje ya Tanzania.
Amesema hayo alipokuwa akitembelea banda la Mradi wa Utafiti wa Akili Unde kwa Afya ya Akili (AI for Mental Health – AI4MH), wakati wa Mkutano wa Pili wa Kisayansi wa UDOM kuhusu Afya (USCHe), uliofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma, Magufuli City, Mtumba – Dodoma.
Pia Prof. Lokina aliipongeza timu ya AI4MH kwa ufanisi na ubunifu wao katika kutumia teknolojia ya Akili Bandia (AI) kuboresha huduma za afya ya akili, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya chuo na wadau wa afya.
Aidha Dkt. Jabhera Matogoro, Mratibu wa Maabara ya Akili Unde kwa Afya ya Akili, alieleza shukrani zake kwa uongozi wa UDOM kwa kuwa bega kwa bega katika utekelezaji wa mradi, na pia akaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia COSTECH kwa kuwezesha mafanikio hayo kwa uwekezaji mkubwa wa kifedha.
Dk. Matogoro aliwahimiza wadau kutoka sekta mbalimbali kuendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Maabara ya AI4MH, ili kuendeleza mbinu bunifu za kutatua changamoto za afya ya akili nchini.
Ikumbukwe Mradi wa AI4MH, unaofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ni mpango wa kitaifa unaolenga kuboresha utambuzi wa mapema, uchunguzi, na msaada kwa changamoto za afya ya akili kupitia teknolojia ya Akili Bandia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED