Madiwani Geita wafurahia usimamizi wa mapato

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:26 PM May 15 2025
Madiwani wa Halmashauri ya Geita
Mpigapicha Wetu
Madiwani wa Halmashauri ya Geita

Baraza la Madiwani la Manispaa ya Geita, limehitimisha muda wake wa miaka mitano ya uongozi kwa kujinasibu na mafanikio makubwa ya kuongeza mapato ya ndani kutoka Sh.bilioni 8 mwaka 2020 hadi Sh. bilioni 19 mwaka 2025.

Meya wa Manispaa ya Geita, Costantine Morand, ameyasema hayo leo Mei 15,2025 katika kikao cha nne cha baraza hilo na kusema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi madhubuti wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa.

“Tulipoanza mwaka 2020 tulikuwa tunakusanya Sh bilioni 8 kwa mwaka, leo tunamaliza tukiwa tunakusanya Sh bilioni 19.Hii inaonyesha kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi chetu,” amesema Morandi.

Mbali na  kuongeza mapato baraza hilo linajivunia kuboresha sekta ya elimu na afya ambapo amaesema wamefanikiwa kuje nga shule mpya,ujenzi wa  vyumba vya madarasa zaidi ya 400 kwa shule za msingi na sekondari, matundu ya vyoo zaidi ya 420, maabara mpya 16 za sayansi, na ongezeko la vituo vya afya kutoka kimoja hadi vitano.

Pia kupitia mapato ya ndani halmshauri hiyo iliweza kuongeza mkopo w aasilimia 10 unaotolewa kwa wanawake,wijana na wenye ulemavu  kutoka Sh. milioni 698 mwaka 2020 hadi kufikia Sh. bilioni 1.78 mwaka 2025.

Aidha, baraza hilo limempongeza, Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, kwa juhudi zake za kukusanya na kusimamia mapato ya ndani ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake mapato ya ndani yameongezeka kutoka Sh bilioni 14 hadi Sh bilioni 19, licha ya halmashauri kutokuwa na vyanzo vipya vya mapato.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amesema sehemu ya mapato hayo ya ndani imeelekezwa kwenye  miradi ya maendeleo ikiwemo elimu,afya,kilimo na biashara.

Amesema kwa robo hii ya nne serikali imetoa zaidi ya Sh.bilioni 3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi ya Tasaf na ujenzi wa kituo cha ualimu.

Kuhusu miradi viporo ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) amesema manispaa imepokea Sh.milioni 204 iliyokamilisha miradi 18 kati ya 34 inayopaswa kukamilishwa .