Sekta ya Uchukuzi yachangia dola bilioni 2.48 za kigeni Julai 2024 – Machi 2025

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 12:46 PM May 15 2025
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, Sekta ya Uchukuzi nchini imechangia kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.48 za fedha za kigeni. Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 8.3 ikilinganishwa na dola bilioni 2.29 zilizopatikana katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2023/2024.

Prof. Mbarawa ametoa taarifa hiyo leo, Mei 15, 2025, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, bungeni jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa Sekta ya Uchukuzi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta nyingine, ikiwemo sekta ya utalii, ambapo mapato ya mauzo ya usafirishaji huainishwa kila mwaka kupitia taarifa ya pamoja inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Waziri huyo amebainisha kuwa mchango wa fedha za kigeni unaotokana na sekta ya uchukuzi unatokana na mapato ya kodi mbalimbali, ikiwemo ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), pamoja na kodi nyingine zinazotokana na bidhaa kama mafuta ya petroli na dizeli.

Aidha, ameeleza kuwa mchango huo pia unatokana na ajira zinazotolewa kwa Watanzania katika shughuli mbalimbali za usafiri na usafirishaji kupitia njia za barabara, reli, maji, na anga, pamoja na shughuli za uendeshaji wa bandari.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa huduma za uchukuzi zimeendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuunganisha sekta mbalimbali na kuwezesha biashara ndani ya nchi, katika ukanda wa Afrika Mashariki, na kimataifa.