Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewataka wavuvi wasiowaaminifu wanaotumia nyavu haramu ambazo haziruhusiwi kuzisalimisha zana hizo kabla operesheni ya kuwakamata haijafanyika.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Uvuvi), Dk. Edwin Mhede ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na baadhi ya wavuvi na wadau wa uvuvi wa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa katika ziara yake ya kufuatilia shughuli za doria zinavyofanyika katika ziwa hilo.
“Ninyi wenyewe wananchi na wavuvi mmesema kwa vinywa vyenu kuwa kuna wavuvi bado wameficha zana haramu za uvuvi majumbani na sehemu mbalimbali, sasa ninawaambia kuwa hizo zana haramu za uvuvi mzisalimishe katika Mamlaka husika ili tuondokane na adha zitokanazo na uvuvi haramu na pia tuwe na uhakika wa uendelevu wa Ziwa letu," amesema Dkt. Mhede.
Naye Mvuvi wa Ziwa Tanganyika, Juma Yahya, akizungumza kwa niaba ya wenzake aliishukru Serikali ya awamu ya sita kwa hatua mbalimbali ambazo imekuwa ikichukua katika kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Tanganyika kwa kutumia nyavu ambazo hazifai.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED