Bunge la Tanzania limepitisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya Sh. trilioni 2.746 kwaajili ya matumizi ya mwaka 2025/26.
Wakati wa hitimisho la Mjadala wa Bajeti hiyo, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amewashukuru wabunge wote 15 waliochangia Mjadala wa Bajeti hiyo, akiahidi kuwa wizara yake itayafanyia kazi maoni, mapendekezo na ushauri uliotolewa, ikiwmo kupunguza kuchelewa kwa safari za ndege zenye kuendeshwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) .
Awali wizara hiyo pia imebainisha kwamba kwa mwaka ujao wa fedha, pamoja na mambo mengine itaendeleza ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR katika ushoroba wa kati, kununua vitendea kazi pamoja na kuboresha reli zilizopo, kuifanyia maboresho ATCL, kuboresha miundombinu na huduma za bandari pamoja na kuendeleza ujenzi wa meli mpya na maboresho ya viwanja vya ndege na Meli zilizopo.
Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, ameipongeza wizara hiyo kwa wasilisho na majukumu ambayo wamekuwa wakiyatekeleza.
Aidha, amemtakia Waziri na Naibu Waziri wake kila lenye kheri katika kutimiza yale yaliyomo kwenye mipango ya wizara kwa mwaka ujao wa fedha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED