Kipindi maarufu cha televisheni Hello Chinese S2 kimeendelea kuvutia watazamaji barani Afrika kwa mbinu yake ya kipekee ya kufundisha lugha ya Kichina kupitia burudani na vikaragosi hai, kikielezwa kuwa daraja jipya la mawasiliano kati ya China na mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania.
Kikiwa katika nusu ya msimu wake wa pili, Hello Chinese S2 ni matokeo ya ushirikiano kati ya StarTimes na Kituo cha Elimu ya Lugha na Ushirikiano cha Wizara ya Elimu ya Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza Dar es Salaam juzi kuhusu kipindi hiko moja ya waratibu wa maudhui wa StarTimes Yuan Zhoung alisema kimeundwa kwa njia ya kuvutia kinachochanganya mafunzo ya lugha ya Mandarin na maudhui ya kiutamaduni ya Kichina, huku kikilenga kuwafikia watazamaji wa rika zote, hasa vijana.
"Ubunifu mkubwa wa kipindi hiki uko katika matumizi ya vikaragosi hai vinavyoonyesha simulizi na matukio ya maisha halisi, changamoto na furaha zinazojitokeza katika kujifunza lugha mpya. Kwa kutumia njia hiyo ya burudani, watazamaji hujifunza misamiati ya Kichina, miundo ya sentensi na matamshi sahihi bila kukinai.
Alisema kuwa kipindi hicho kimebuniwa ili kufanya lugha ya Kichina kuwa rafiki kwa watazamaji wa Afrika. Kipindi hiko hurushwa kupitia chaneli mbalimbali kama ST Sino Drama Jumatano hadi Jumapili, ST Guide E: Jumatatu hadi Ijumaa
“Tunafundisha lugha kupitia burudani na tunahakikisha kila kipindi kinatoa msamiati wa msingi pamoja na maarifa ya kiutamaduni — kutoka sherehe za jadi hadi uvumbuzi wa kisasa,” alisema.
Mbali na vikaragosi, Hello Chinese S2 pia huangazia tamaduni mbalimbali za Wachina, zikiwemo Sherehe Kwaza Mwaka Mpya wa Kichina, Tamasha la Taa, sanaa ya uchoraji kwa wino, na uandishi wa Kichina wa jadi. Maudhui haya yanatoa mwanga kuhusu maisha ya Kichina ya sasa na ya kale, na mabadiliko yanayoendelea katika jamii yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED