Matumizi ya dawa za kuzuia wadudu, manukato , vyakula vya kopo na runinga,vimetajwa kuwa chanzo cha tatizo la usonji kwa watoto.
Mtafiti na Bingwa wa Watoto, Profesa Karimu Manji, alitoa kauli hiyo jana akiwasilisha utafiti wake kuhusu Usonji, wakati wa Kongamano la 13 la Kisayansi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam.
Prof. Manji alisema utafiti aliufanya amebaini matumizi ya dawa za kupuliza kuua wadudu na kupata manukato zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibu ubongo wa mtoto hivyo kusababisha usonji.
Aidha matumizi ya simu janja, vishikwambi na runinga ambazo zinatumiwa na wazazi kama njia ya kuwaburudisha au kuwanyamazisha inachangia pia.
“Matumizi hayo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano yana athari kubwa kiafya na kusababisha usonji, mtindo wa malezi kwa wazazi na walezi umebadilika sana, siku hizo wanatumia runinga na mitandao ya kijamii kuwanyamazisha watoto au kuwaburusha ili waendelee na majukumu yao,” alisema Prof. Manji.
Aliwashauri wazazi na walezi kutumia vitu hivyo kwa uangalifu, alitoa takwimu kuwa kati wa watoto 150 mmoja ana tatizo la usonji kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2022.
Alitaja baadhi ya dalili kwa watoto wenye usonji kuwa ni kushindwa kutamka maneno kwa ufasaha au kurudia vitu visivyoeleweka, kuona aibu wakati kuzungumza na hisia au tabia hasi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza ya Afya ya Akili, kutoka Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubugoyu, alisema serikali imekusudia kuongeza juhudi za ugunduzi wa mapema wa usonji kupitia vituo vya afya na shule.
Wameanzia Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha programu kwenye shule 100 za awali, ambapo zaidi ya walimu 4,000 watafundishwa namna ya kutambua dalili za usonji kwa watoto.
Aliongeza kuwa wameongeza mafunzo kwa wahudumu wa afya ili kuwawezesha kutoa huduma za kitaalamu kwa watoto wenye changamoto hiyo tayari wataalamu 50 wamehitimu.
Profesa Appolinary Kamuhabwa, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa alisema wameanzisha shahada mpya zinazolenga kusaidia watoto wenye matatizo ya usonji, ikiwa ni pamoja na Physiotherapy, Speech Therapy, na taaluma ya kusaidia watoto wenye matatizo ya viungo.
Naye Naibu Makamu wa MUHAS anayeshughulikia Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Bruno Sunguya, alisema mwezi Aprili ni maalum kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu usonji.
“Mtoto mwenye usonji si mlemavu, akigundulika mapema na kupata matibabu anaweza kubadilika na kuwa mtaalamu mahiri na wa kuaminika katika jamii,” alisema Prof. Sunguya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED