Mshitakiwa adai hajapona akili kesi isiendelee

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 01:45 PM Apr 11 2025

Mhandisi Faustine Malya (44).
Picha: Grace Gurisha
Mhandisi Faustine Malya (44).

Mhandisi Faustine Malya (44) anayetuhumiwa kujipatia zaidi ya Sh. milioni 300 kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali kwa njia ya udanganyifu ameieleza mahakama kwamba hawezi kuendelea kusikiliza kesi kwa sababu akili yake inaweza ikafyatuka, bado hajapona afya yake ya akili.

Aidha, upande wa Jamhuri umedai kwamba anachokifanya Malya ni kuchelewesha kesi kwa sababu tayari ripoti ya daktari inaeleza kuwa afya yake imetengeemaa, amebakiza matibabu ya nje ya kuzungumza na wanasaikolojia.

Mshtakiwa Malya alidai hayo juzi mbele ya Hakimu Mkazi, Amos Rweikiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kughushi ilipoitwa kwa ajili kusikilizwa kwa mashahidi wa Jamhuri.

"Siwezi kuendelea na kesi kwa sababu ya hali yangu ya kiafya cheti hiki hapa (anaonesha) halisi na nakala ni kweli naendelea vizuri tofauti na awali nilikuwa napiga watu hata hapa kichwa kinaweza kikacheza akili ikatoka,"

"Nilipokuwa gerezani nilikuwa napiga wenzangu hadi nikafungiwa kwenye chumba maalum kwa hiyo mimi na daktari ndiyo tunajua hali ya akili yangu," amedai Malya

Pia, kwa upande wa mawakili wa washtakiwa wengine Peter Shapa na Pharis Mshana na wao waligoma kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo na kudai kuwa wanataka haki itendeke kwa kila upande kwa kukaa kwanza na wateja wao.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Burton Mayage akisaidiana na Janeth Kimambo amedai kuwa hoja hizo hazina mashiko za kusababisha kesi iahirishwe kwa sababu walikuwa na muda mrefu wa kutafuta wakili tangu kesi ilipoahirishwa mara ya mwisho Machi 28,2025.

Alidai kuwa Wakili Mshana alikuwa na jukumu la alifuatilie 'follow up ' mahakamani ili ajue nini kinachoendelea, hakuna sababu ya kutokuendelea na usikilizwaji kwa sababu shahidi amefika mara ya tatu lakini hatoi ushahidi wake.

Kuhusu hoja ya mshtakiwa Malya kwamba hana wakili, Mayage amedai ni njia ya kuchelewesha kesi kwa sababu taarifa ya daktari inaonesha kwamba afya yake ya akili imetengemaa, isipokuwa kilichobaki ni matibabu ya nje ya kuzungumza na wanasaikolojia.

"Tathimini yake ya afya ya akili inaendelea kuimarika kwa hiyo hana sababu ya msingi ya kesi hii kuahirishwa. Naomba tuendelee na usikilizwaji ni mara ya tatu shahidi anarudi bila kutoa ushahidi,"amedai Wakili Mayage.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Rweikiza ametoa amri kwamba Mei 13,2025 washtakiwa wote wawepo na kesi itasikilizwa haitaahirisha tena usikilizwaji tutaendelea na pia amezingatia hoja za upande wa utetezi.