Mwalimu, rafikiye wadaiwa kubaka mwanafunzi

By Rose Jacob , Nipashe
Published at 02:40 PM Mar 20 2025
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbrod Mutafungwa.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbrod Mutafungwa.

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, linawashikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Bukalu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na rafiki yake kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wake wa kike mwenye umri wa miaka 10.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbrod Mutafungwa alisema kuwa tukio la mwanafunzi huyo kubakwa na watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti tangu mwaka jana, liligundulika mwezi uliopita baada ya kudhoofika kiafya.  

Mutafungwa, alisema inadaiwa kuwa watuhumiwa hao walimbaka mwanafunzi huyo kati ya Oktoba 24, mwaka jana hadi Februari 2025 katika nyumba anayoishi rafiki wa mwalimu huyo. 

Alisema mwalimu huyo inadaiwa kuwa  alimuita mwanafunzi huyo nyumbani kwake mwezi uliopita kwa kisingizio cha kumfundisha masomo ya ziada na kumbaka. 

Kamanda huyo, alisema kwa mujibu wa mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Februari 26, mwaka huu, asubuhi alibaini kuwa mtoto huyo afya yake imedhoofika na kuamua kumpeleka hospitali. 

Alisema mama huyo alidai baada ya daktari kumfanyia uchunguzi mwanae huyo alibaini kuwa na michubuko sehemu za siri kutokana na kubakwa. 

“ Hivyo mama huyo aliamua kutoa taarifa katika kituo cha Polisi Sengerema. Uchunguzi ulianza siku hiyo na Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani,” alisema Mutafungwa. 

Akizungumia tukio jingine; Mutafungwa, alisema mwalimu wa Shule ya Msingi Nyampande anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Nyampande (16).

 Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumbaka mwanafunzi huyo  Februari 24, mwaka huu asubuhi katika Kijiji cha Nyampande wakati akiangalia mpira wa miguu nyumbani kwake.

 â€śInadaiwa mwanafunzi huyo alikuwa na desturi ya kwenda kutazama televisheni nyumbani kwa mwalimu huyo na siku hiyo ndipo alipomfanyia ukatili huo,” alisema Kamanda huyo.

 Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka baada ya upelelezi kukamilika.